*Ni baada ya Serikali kusikia kilio kutoka kwa wafanyabiashara
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeanza jitihada za kufuta tozo zote ambazo zinakwamisha mazingira ya ufanyaji wa biashara nchini zikiwemo za kwenye pembejeo ili kuwawezesha wafanyabiashara kuzifikisha hadi ngazi ya kijiji kwa wakulima.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei 23, 2019) Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Madaba, Kizito Mhagama katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kupunguza tozo kwa maduka yanayouza pembejeo ili kumwezesha mkulima kupata pembejeo.
Waziri Mkuu amesema Serikali imepokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo na wauzaji wa pembejeo juu ya tozo mbalimbali katika uendeshaji wa shughuli nzima wa biasharazao.
“Serikali imesikia vilio vyenu na sasa inafanya mapitio ya tozo hizo na itakapofikia hatua nzuri itawajulisha na kuwashirikisha kujua ni aina gani ya tozo ambayo itaondolewa au kuibadilisha ili muendelee kufanya biashara zenu katika mazingira rahisi.”
Waziri Mkuu amesema kazi kubwa inayofanywa na Serikali kwa sasa ni kufanya mapitio ya tozo zote kuanzia kwa wakulima hadi kwa wafanyabiashara na kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara nchini, ikiwemo ya pembejeo ili kuzifikisha kiurahisi kwa wakulima.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kwamba tayari Mawaziri wa kisekta wenye dhamana ambao wana tozo mbalimbali kwenye wizara zao zinazokwamisha ufanyaji biashara katika mazingira rafiki wameshakutana kwa ajili ya kujadili namna ya kulipatia ufumbuzi suala hilo.
“Hata juzi nilikuwa na mawaziri hao kupata taarifa zao kwa pamoja kuona maeneo yote waliyoyapitia na tozo zote zinazokusudiwa kupitiwa upya na kazi hiyo ikikamilika watakutana na Kamati ya Bajeti ya Bunge, Wizara ya Fedha ili kuona namna nzuri ya kuondoa tozo hizo. Lakini baadaye suala hilo litaenda kwenye mamlaka inayotoa ridhaa ya kuondoa au kupunguza tozo.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema miradi mingi ya maji ambayo inatekelezwa kwenye maeneo mbalimbali nchini baadhi yake haitekelezwi kwa viwango vilivyokusudiwa, hivyo haiwiani na thamani halisi ya kiasi cha fedha kinachotolewa.
Hata hivyo Waziri wa Maji wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2019/2020 alieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa dhidi ya miradi yote ambayo haiwiani na kiasi cha fedha kilichotolewa pamoja na hatua zilizochukuliwa dhidi ya miradi yote.
“Moja kati ya hatua ambazo amezifanya ni pamoja na kuunda timu inayopita kukagua miradi yote nchini na kujiridhisha kama matengenezo yake yanakidhi thamani ya fedha iliyotolewa katika mradi huo na kama haukidhi hatua kali zinachukuliwa kwa wahusika.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa Korogwe Mjini Mary Chatanda aliyetaka kujua Serikali kama ipo tayari kuchunguza na kuchukua hatua kwa watendaji walioshindwa kusimamia miradi ya maji na kuisababishia hasara pamoja na wananchi kukosa huduma waliyokusudiwa.