Mchezaji wa timu ya Transit Camp ya Daraja la Kwanza Ahmad Waziri (pichani) amefariki ghafla asubuhi ya leo baada ya kudondoka akiwa anatoka mazoezini na wenzake kwenye Kambi ya Twalipo, Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Taarifa zinaeleza kuwa Ahmad akiwa na wenzake wakielekea kupanda daladala maeneo ya Uhasibu, aliinama kama anafunga kamba za viatu, akapata kizunguzungu na kuanguka ghafla na ndipo wenzake wakachukua usafiri wa bajaji na kumkimbiza hospitali.

Ahmad amewahi pia kuzichezea Simba SC, African Lyon, Majimaji FC, Mlale JKT na JKT Tanzania na kwa kipindi hiki alikuwa akiitumikia Transit Camp ambayo inajiandaa kwaajili ya mechi za ‘play-off’, ili kujinusuru kushuka daraja.