Spika wa Bunge Job Ndugai, amesema Mbunge wa Shinyanga Mjini Stephen Masele, hawezi kukaidi tena agizo la kutakiwa kufika Kamati ya Maadili baada ya kuitwa na Spika huyo kwa mara ya pili.

Akizungumza na waandishi wa habari Spika Ndugai amesema suala la Bunge kumuita Masele halihusiani na matukio yaliyotokea Afrika Kusini bali ni kwa sababu ya mambo aliyofanya nyumbani.

"Ameitwa kwa mambo ya hapa nyumbani ya utovu wa nidhamu, anaunganisha hilo na matendo anayoyafanya huko, lakini hatujamuita kwa mambo ya South Afrika Watanzania watulie baada ya muda zitaletwa bungeni kila mtu atasikia kuhusu anatuhumiwa nini na majibu yake yalikuwa nini na wataelewa kama ameonewa au hajaonewa.

"Stephen Masele hawezi kukaidi zaidi kwa sababu ni lazima arudi Tanzania, labda sababu awe mkimbizi na  akirudi Tanzania lazima aje Kamati ya Maadili, ni wito wa kisheria tunachomuitia ni tabia yake uchonganishi wa viongozi, kwa sasa hatuwezi kusema ila akishatoka mtaelewa fitina ikoje, ambayo ni kukosa sifa kwa kiongozi yeyote yule", amesema Spika Ndugai.