DAR ES SALAAM: Skendo mbichi ya unga inamhusu mjasiriamali maarufu jijini Dar es Salaam, Shamim Mwasa na mumewe Abdul Nsembo hivi karibuni kunaswa kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin.UWAZI limebaini kuwa, kudakwa kwa Shamim ambaye ni mtangazaji, mwanamitindo, mbunifu wa mavazi na mhamasishaji wanawake kimaendeleo, kumemuibua mrembo mwingine Mbongo, Jacqueline Patrick ‘Jack’ aliyekamatwa nchini China kwa madawa ya kulevya kisha kufungwa miaka 6 jela.Shamim na Jack wamewekwa kapu moja si kwa sababu nyingine, bali katika mjadala mzito unaoendelea mitandaoni kuhusu kuhusika au kutokuhusika kwa mke huyo wa Nsembo anayedaiwa kuwa ni papa wa biashara ya dawa za kulevya. 
HOJA MOTO MITANDAONI

Tangu kukamatwa kwa Shamim na mumewe Mei Mosi, mwaka huu kwa tuhuma hizo, hoja moto zilizopo mitandaoni ni aina ya maisha waliyokuwa wanaishi Shamim na Jack Patrick. Jack kabla ya kukamatwa kwa unga China alionekana kuwa ni mwanamke mwenye mafanikio kama ilivyo kwa Shamim ambaye amekuwa akijishughulisha na mambo ya ujasiriamali.“Shamim labda awe ameponzwa na mume wake, mtu ana biashara zake kubwa tu, auze madawa ya kulevya ili iweje?” Mwanamke mmoja alitoa hoja yake kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram kulikokuwa kukijadiliwa habari ya kukamatwa kwa Shamim na mumewe kwa tuhuma hizo nzito.

WENGI WAMSIKITIKIA SHAMIM

Hata hivyo, uchunguzi unaonesha kuwa watu wengi hasa wanawake wamekuwa wakimtetea Shamim kuwa hawezi kuwa anahusika na biashara hiyo na kujaribu kumsukumia mzigo huo wa tuhuma mumewe Nsembo. Wengi kati ya waliomtetea walisema mara nyingi wanawake wamekuwa wakijikuta matatani kwa kusababishiwa na waume wao. “Sisi wanawake ni vigumu mno kututenga na uhalifu wa waume zetu, unaweza kukuta hujui kama mumeo anafanya biashara ya madawa ya kulevya.“Na si hilo tu anaweza kuwa jambazi, lakini si kwamba wewe unashirikiana naye, lakini siku akija kukamatwa unajikuta nawe unaingia mtegoni bila kujua. “Hiki ndicho naamini kimemkuta Shamim,” alisema Agness Daniel, mkazi wa Sinza-Madukani, Dar alipokuwa akitoa mawazo yake mbele ya UWAZI lililotaka kujua anachukuliaje skendo ya Shamim kukamatwa kwa tuhuma hizo za unga.Wakati mawazo kama hayo yakiendelea mitaani, kwenye mitandao ya kijamii mambo yalikuwa ni yaleyale ya kuwepo kwa uwezekano wa mwanamke kuponzwa na uhalifu wa mumewe jambo ambalo lilimfanya mwandishi wetu awasiliane na Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya ‘DCEA’ ili kupata somo. Majibu yaliyotafutwa na mwandishi wetu ni kuwepo kwa uwezekano wa Shamim kuingizwa kwenye skendo ambayo hahusiki nayo na kwamba ameponzwa na kuwa mke wa mtuhumiwa yaani mumewe Nsembo.


MAHOJIANO NA DCEA HAYA HAPA

UWAZI: Naongea na afisa habari wa mamlaka ya madawa ya kulevya?

DCEA: Hapana, ila ni mmoja wa maofisa, unapenda kusaidiwa nini?

UWAZI: Kuna hii habari ya kukamatwa kwa Shamim na mumewe kuhusu dawa za kulevya nadhani tukio unalijua?

DCEA: Ndiyo nalijua, lakini kwa kuwa liko kwenye mamlaka ya juu, mimi siwezi kulizungumzia.

UWAZI: Ok, hilo tunaweza kuliweka kando kwa sababu limeshajulikana, nilichotaka kujua ni kuhusu uwezekano wa mwanamke kukamatwa kwa kosa la mumewe, maana hicho ndicho kinachoelezwa mitandaoni hivi sasa.

DCEA: Sijakuelewa unamaanisha Shamim kakamatwa kwa kosa la mumewe?

UWAZI: Hapana, sisemi Shamim; nadhani tumekubaliana hilo tusilizungumzie ninachotaka ni elimu kwamba mwanamke anaweza kuwekwa kwenye mkumbo wa mtuhumiwa mfano, mumewe akiwa ni jambazi, mara Polisi wanakuta bunduki ndani ambako mke pia analala hili huoni linaweza kuwa jambo la kuleteana shida kwa kupitia ndoa?

MAMBO MATATU YATAJWA

Kutokana na mahojiano hayo afisa huyo wa DECA aliliambia UWAZI kuwa, ili mwanamke aweze kuepuka kile kinachoitwa kukumbwa na mkumbo wa kihalifu ni lazima mambo matatu yafanyike ili kujiokoa. “Wanawake wanatakiwa kujua kuwa ni vigumu kwao kukwepa mkono wa sheria kwa kusingizia mkumbo, wanachotakiwa kufanya ni kujitenga na mkondo wa kihalifu.“Kwanza, kama mwanamke anajua na off course lazima ajue kuwa mumewe anafanya biashara haramu, anachotakiwa cha kwanza ni kumkataza aachane nazo. “Pili, kama hakuachana nazo asiendelee kuishi naye kimyakimya, anatakiwa kumripoti kwenye vyombo vya dola ili mzigo umhusu anayetenda peke yake.“Akiona hawezi kufanya hivyo basi ni vyema akaikacha ndoa yake na kumwacha mumewe na makosa yake, siku akikamatwa mzigo utakuwa wake,” alisema afisa huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa sababu ya madai kuwa suala la Shamim na mumewe lilikuwa kwenye ngazi za juu za DCEA.MWANASHERIA ANENA

“Hakuna haja ya kupiga kelele juu ya kuhusika kwa mtu au kutohusika kwa sababu chombo kinachoweza kuthitisha hayo ni mahakama. “Na mahakama haimhukumu mtu kwa sababu tu kakamatwa na Polisi au vyombo vingine vya usalama, mahakama inahukumu kwa ushahidi usiokuwa na shaka kuwa anachotuhumiwa nacho mtu alikitenda au la,” alisema wakili wa kujitegemea Fredy Mongi wa Kimara, Dar.TUJIKUMBUSHE

Shamim na mumewe ambao ni wakazi wa Mbezi-Beach, Dar walikamatwa hivi karibuni wakituhumiwa kukutwa kiasi cha gramu kati ya 560 hadi 700 za madawa hayo ya kulevya, hiyo ni kwa mujibu wa Kamishna wa Oparesheni wa DCEA, Luteni Kanali Fredrick Milanzi. Tangu kipindi hicho watuhumiwa hao wako mikononi mwa vyombo vya usalama na kwa mujibu wa Luteni Kanali Milanzi upelelezi mkali unaendelea dhidi yao