Licha ya kuwepo kwa matamko kutoka Yanga kuwa mchezaji wao Ibrahim Ajibu ataendelea kusalia klabuni kwao, watani zao wa jadi wameonesha jeuri ya pesa wakitaka kumsajili.

Ofisa Habari wa klabu ya Simba ameibuka na kueleza kuwa bado hawamsajili Ajibu lakini kama yupo kwenye ripoti ya Kocha Patrick Aussems hakuna namna ya Yanga kumzuia tena.

Manara ametemba kwa kusema wana jeuri ya pesa hivi sasa kutokana na kuwa kwenye mchakato wa mabadiliko ulio chini ya Mwekezaji wao Mohammed Dewji Mo.

Ofisa huyo amefunguka akisema Simba haiwezi kushindwa kumsajili Ajibu kwakuwa kila mchezaji hivi sasa anatamani kujiunga na mabingwa hao wa mwisho wa mara mbili mfululizo katika Ligi Kuu Bara.

"Kama atakuwa katika ripoti ya Mwalimu wetu wala hatutashindwa kumsajili, ila kwa sasa siwezi kusema lolote, tusubiri muda ufike."

Licha ya Manara kusema hivyo, taarifa za ndani zinasema tayari mchezaji huyo kashamwaga wino ndani ya wekundu hao wa Msimbazi uliogharimu kitita cha milioni 80.