JUMLA ya shilingi Milioni 400 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Mapera kata ya Mapera Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ambrose Mtarazaki amesema hayo jana wakati akifungua kikao cha Baraza la robo ya tatu cha Baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Umati Mjini Mbinga.

Alisema, ujenzi wa kituo hicho utakapokamilika utasaidia sana kuwaondolea wananchi wa kata ya Mapera na Bonde zima la Hagati kusafiri umbali mrefu hadi Hospitali ya wilaya iliyopo Mbinga Mjini au Hospitali ya Misheni Litembo kufuata matibabu.

Mtarazaki ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kutoa fedha hizo ambazo zitakwenda kukamilisha kazi hiyo na kuimarisha huduma za Afya kwa wananchi hasa ikizingatia kuwa, lengo la kujenga kituo cha Afya Mapera ni la muda mrefu hata hivyo walishindwa kutokana na ukosefu wa fedha.

Amewaomba wananchi wa Mapera na kata jirani kuhakikisha wanashiriki vema katika ujenzi wa miundombinu kwa kupeleka mchanga ,tofali na mahitaji mengine ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati badala ya kuiachia Serikali jambo linalo weza kuchelewesha kazi hiyo.

Aidha Mtarazaki, ametaka fedha hizo zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwaonya watendaji wa Serikali kanzia ngazi ya kijiji hadi wilaya kutothubutu kwa namna yoyote kujaribu kutumia fedha hizo kinyume na malengo.

Katika hatua nyingine Mtarazaki alisema, katika kipindi cha robo ya tatu ya Mwaka wa Fedha 2019/2020 Halmashauri ya wilaya imeweza kutekeleza na kufuatilia miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo mbalimbali hatua iliyochochea sana upatikanaji wa huduma bora za kijamii kwa Wananchi.

lisema, katika kipindi hicho Halmashauri ya wilaya imetoa shilingi Milioni 261 kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa na Upimaji na usimamizi wa matumizi Bora ya Ardhi katika vijiji mbalimbali.

Mtarazaki alisema, pia Halmashauri ya wilaya imetoa jumla ya shilingi milioni 198 kama mkopo kwa makundi maalum ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu pamoja na shilingi milioni285 zilizotengwa kwa ajli ya ununuzi wa magari mawili ili kurahisisha utendaji wa watumishi na utoaji huduma Bora kwa wananchi.

Alisema, sambamba na hilo Halmashauri imefanikiwa kupata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG),na amewataka watumishi wa Halmashauri ya kuendelea kufanya kazi kwa weledi na madiwani kuhakikisha wanasimamia kikamilifu vyanzo vyote vya mapato ili fedha zinazokusanywa ziende kufanya kazi ya kumaliza changamoto na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Pi aliwaeleza madiwani kuwa,hadi kufikia mwezi April mwaka huu Halmashauri imeshakusanya asilimia 85 ya mapato yake ya ndani.

Hata hivyo alisema, licha ya mafanikio hayo bado kuna tatizo kubwa kwa baadhi ya watendaji wachache kushindwa kutumia mashine za POS kwa ajili ya kukusanya mapato ya Halmashauri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Juma Mnwele akifafanua jambo kwa wajumbe wa Baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Umati Mbinga,katikati Mwenyekiti wa halmashauri Ambrose Mtarazaki.