BAADA ya kusambaa kwa taarifa nyingi kuhusu ndoa yake mitandaoni, hatimaye mrembo kutoka Bongo Movies, Shamsa Ford, amekiri kumwagana na mumewe Rashid Said ‘Chid Mapenzi’.



Taarifa za Shamsa kumwagana na mumewe zilianza kusambaa katikati ya wiki hii ambapo kwenye mitandao ya kijamii hususan Instagram, kila mmoja alisema lake.



Kuna ambao walisema ni kweli wameachana lakini kuna wengine walisema taarifa hizo hazina ukweli wowote. “Jamani hawajaachana, anaweka tu comments zenye utata ndio zinazowafanya watu waseme wameachana,” alichangia mdau mmoja mtandaoni.



Mwingine akasema: “jamani mimi kuna mtu yupo karibu sana na Shamsa kanimegea kabisa kwamba ndoa yao imeshaota mbawa.”



Baada ya maneno kuwa mengi, mwanahabari wetu alilazimika kumtafuta Shamsa kupitia simu yake ya mkononi ambapo alipopatikana alikiri kuachana na mumewe lakini hakuwa tayari kuzungumzia zaidi suala hilo.



“Ni kweli lakini nisingependa kuongea lolote kwa sasa, tafadhali sana naomba mniache,” alisema Shamsa.



TULIPOTOKA

Kabla ya wawili hao kumwagana, walikuwa wakioneshana mahaba ya kufa mtu kwenye mitandao ya kijamii. Mara kadhaa wakati Chid alipokuwa akisafiri nje ya nchi kibiashara, Shamsa alionekana kumwaga machozi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar anapokuwa amemsindikiza.



Mwaka 2016, Shamsa aliolewa na Chid ambaye ni mfanyabiashara, ambapo ndoa yao ilikuwa gumzo kwani kabla ya hapo, mrembo huyo alikuwa kwenye uchumba wa muda mrefu na mwanaume aliyefahamika kwa jina la Dickson Matoke ambaye alizaa naye mtoto mmoja wa kiume, Terry.



Shamsa ametengana na mumewe, ikiwa ni siku chache tangu ilipothibitika kuwa, penzi la msanii mwenzake wa filamu, Aunt Ezekiel na densa maarufu wa WCB, Mose Iyobo limevunjika.

SHAMSA FORD NI NANI?

Ni msanii wa kitambo kwenye Bongo Muvi, akianzia kwenye kundi maarufu la sanaa la Kaole, lakini alikuja kupata umaarufu zaidi alipoanza kushiriki sinema za Kibongo.

Ameshiriki sinema nyingi za wasanii wakubwa na wachanga, lakini zilizompaisha zaidi ni Saturday Morning aliyocheza na marehemu Steven Kanumba, Bado Natafuta akiwa na Salim Ahmed ‘Gabo’ na Zawadi ya Birthday aliyoshiriki na Jacob Stephen ‘JB’.