MKURUGENZI na Msemaji Mkuu wa, Dkt. Hassan Abbasi amesema Serikali inaendelea na majadiliano kuhusu kuendelea na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo Mkoani Pwani ili kuona kama inaweza kuwa na tija kiuchumi kwa upande wa Tanzania.

Dkt. Abbasi alisema Serikali ina uwezo wa kujenga bandari nyingi na kwa kuwa Tanzania ina ukanda mkubwa wa ufukwe wa bahari na kwamba bado majadiliano yenye tija kwa Taifa yanaendelea kufanywa baina ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji wa mradi huo.

“Serikali haijasema kuwa Mradi wa Bandari ya Bagamoyo ni hatari, tunaendelea na majadiliano ya utekelezaji wa mradi huo, nchi yetu imejaliwa ukanda mkubwa wa ufukwe wa bahari kwa hiyo tuna uwezo wa kujenga Bandari nyingi tu, hii ya Bagamoyo si kweli kuwa imeachwa kuna mambo ya msingi tunayajadili na tusipofikia maamuzi tutaachana nayo” alisema Dkt Abbasi.

Kuhusu suala la uwekezaji wa vitu aliloulizwa kwenye kipindi hicho Dr Abbasi alisema Serikali haitaacha kuwekeza kwenye vitu kwa sababu vitu husaidia maendeleo ya watu, mfano afya, elimu na miundombinu mingine.

“Kwenye sekta ya madini tumekuachia fedha, dawa hospitalini tumeongeza na bei zimepungua, tumekuletea yote hayo lakini bado unasema huna pesa mfukoni, Serikali inafanya yote haya kuhakikisha kuwa uchumi wetu unaleta manufaa mapana kwa Taifa” alisema Dkt. Abbasi.

Kuhusu uhuru wa Habari na kufungia magazeti yasiyofuata sheria za uchapishaji Msemaji huyo wa Serikali alisema kuwa ofisi yake haikurupuki  kufungia magazeti, na kusema kuwa  ni magazeti  mitatu tu yalifungiwa kati ya 266 yaliyosajiliwa nchini na kuwataka wamiliki wa magazeti hayo kufuata sheria.

Kuhusu malamiko ya wafanyabiashara kwenye maeneo mbalimbali nchini ya kufunga biashara hizo kwa kisingizio cha kodi na tozo mbalimbali, Dkt. Abbasi alisema ni muhimu wakaelewa kwamba kwa sasa Serikali inapita katika kipindi cha mabadiliko na hakuna siku serikali haitadai kodi huku akieleza kuwa kodi nyingi zimepunguzwa hususan kwenye sekta za Kilimo, Mifugo na uvuvi.

“Kwanza tukubali tunapita kwenye kipindi cha mabadiliko, hakuna siku serikali haitadai kodi kwa sababu ndio msingi wa maendeleo ya nchi hii, kuna dhana ilijengeka kuwa unaweza kufanya biashara bila kulipa kodi hiyo sasa haipo, lazima tuangalie changamoto ambazo zinakumba sekta mbalimbali mfano sekta ya kilimo, miufgo na uvubvi kulikuwa na kodi zaidi ya 150, serikali imefuta zaidi ya kodi 80 hadi 100” alisema Dkt Abbasi