Serikali yaeleza kilichotokea kwa kujenga ukuta
Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amesema uboreshaji na uendeshaji kwenye sekta ya madini kwa miaka mitatu umeleta mafanikio makubwa ikiwemo ongezeko la mapato kutoka bil. 201 kwa mwaka 2015/2016 mpaka bil. 302, kwa mwaka 2019.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Dkt.Abbasi amesema kudhibiti utoroshwaji wa  madini ikiwemo ujenzi wa ukuta wa Mererani na uanzishwaji wa masoko kumeipatia heshima Tanzania kuwa kinara wa ulinzi wa rasirimali za nchi kwa bara la Afrika.

"Nchi yetu imepata heshima kubwa duniani, imekuwa ya mfano kwa kusimamia madini, Duniani kote unasikia tuachokifanya ni nchi ya kwanza kuwabana wakubwa, hata yule mwenzetu aliyekwenda BBC akaponda yanayotokea akakutana na yaliyomkuta, mwandishi mwenyewe anaufahamu yanayotokea Tanzania",  amesema Dkt Abbasi.

"Ulijengwa ukuta Mererani watu wakakimbilia mtandaoni ukuta utasaidia nini,  niseme tu Serikali hii inaongozwa Kisayansi, kuna Sayansi na Sanaa kinachowasumbua wengi ni kitu kipya, kuna Sayansi ya kuongoza nchi tangu tujenge mapato na uzalishaji wa madini umeongezeka, unaweza ukabeza ukuta lakini hii ndiyo sayansi tangu tuujenge ukuta", ameongeza Dkt Abbasi.

Aidha Dk.Abbasi amezungumzia ziara alizofanya Rais Magufuli kwa baadhi ya nchi jirani ambapo amesema, "ziara hii Rais ameifanya ikiwa ni maandalizi ya kuchukua Uenyekiti wa SADC Julai mwaka huu, na Agosti tutakuwa na mkutano wa Marais wa SADC na Tanzania itakuwa mwenyeji, alikwenda Namibia kukutana na Mwenyekiti anayemaliza muda wake, mara ya mwisho Tanzania kushika uenyekiti SADC ilikuwa miaka 16 iliyopita".