Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini amemshauri Spika Job Ndugai  kuunda kamati ya wabunge wachache ikague maghala ya kuhifadhi korosho ili kubaini nzima na zilizooza.

Kaimu Mnadhimu huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Mei 20, 2019 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka 2019/2020.

Huku akimsifu Ndugai kwa kuunda kamati zilizochunguza masuala mbalimbali ikiwemo ya madini ya Tanzanite, Selasini amesema, “Nimeitazama picha ya Rais akiwa ameshika paji la uso anaonyesha kutafakari sana.

“Inaonekana Rais ana mawazo mengi. Kazi ya Bunge hili ni kuishauri Serikali. Kazi ya Bunge hili ni kuisimamia Serikali tunafanya makosa makubwa sana kufanya siasa ndani ya Bunge hili.”

Huku akieleza kuwa yeye ni msafirishaji wa korosho, amesema zao hilo huoza kama  vitunguu

“Nimetangulia kukusifu Spika kama kuna ubishi wa korosho zimeoza ama hazijaoza tengeneza kamati ya watu wachache waende wakague kwenye maghala. Nataka nikwambie kuwa korosho imeoza kwa asilimia 30. Weka watu wakakague maana tukiendelea kuzubaa hata zilizopo zitaoza tutapata hasara zaidi.”