Afisa maendeleo wa halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama Aminael John, akielezea madhara ya mimba na ndoa za utotoni kuwa athari zake kuwa ni ongezeko la vifo vitokanavyo na uzazi, kuugua fistula, pamoja na magonjwa mengine ya ikiwa via vyao vya uzazi vinakuwa bado havijakomaa.

Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Shinyanga Save The Children na KIWOHEDE, yameendesha Tamasha Mwanaume Jasiri la Kupinga Mila na Desturi kandamizi katika Kata ya Ulowa halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, kwa lengo la kutokomeza mimba na ndoa za utotoni.


Tamasha hilo limefanyika Alhamis Mei 16, 2019 katika kijiji cha Kangeme Kata ya Ulowa, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Afisa Maendeleo Jamii wa halmashauri ya Ushetu Aminael John akimwakilisha mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha.


Tamasha hilo liliambatana na kauli mbiu isemayo “Mwanaume Jasiri ana mlinda mtoto wa kike dhidi ya mimba na ndoa za utoton”.


Akizungumza kwenye Tamasha hilo mgeni rasmi Afisa Maendeleo wa halmashauri  ya Ushetu Aminael John, amewataka wanaume kuacha kuendekeza mila na desturi kandamizi zilizopitwa na wakati, ambazo zimekuwa zikichangia kuendelea kuwepo kwa tatizo la mimba na ndoa za utotoni.


Amesema wanaume wanatakiwa kubadilika na kutambua umuhimu wa elimu, kwa kumlinda mtoto wa kike dhidi ya matukio hayo ya kupewa ujauzito na kuolewa ndoa za utotoni, ili waweze kutimiza malengo yao na kuja kuwasaidia hapo baadae.


“Natoa wito kwa wanaume wa kata hii ya Ulowa na Ushetu kwa ujumla, acheni kuendekeza mila na desturi kandamizi ambazo zimekuwa zikiwanyima haki watoto wa kike kuweza kutimiza malengo yao, na kuishia kupewa ujauzito ama kuolewa ndoa za utotoni na kuacha shule,”amesema John.


“Tambueni kuwa mtoto anapopata elimu ataweza kuja kuwa kiongozi mkubwa hapa nchini au kupata ajira yake nzuri, ambapo atawasaidia katika maisha yenu kuliko hata hao ng’ombe mnawategemea na kuona wa thamani sana, na kuamua kuwaozesha ndoa hizo za utotoni kwa tamaa ya kupata mifugo,”ameongeza.


Naye Mtendaji wa kata ya Ulowa Geofrey Philip, ametaja takwimu za wanafunzi ambao walikatishwa masomo mwaka jana (2018) kwa sababu ya kupewa ujauzito kuwa walikuwa 10, ambapo kwa mwaka huu (2019) tayari wameshapewa mimba wanafunzi wawili.


Aidha Kaimu Mkurugenzi wa shirika la Save The Children mkoa wa Shinyanga Alex Enock, amesema wameanzisha mradi huo katika kata nane za halmashauri hiyo ya Ushetu, kwa lengo la kutokomeza mila na desturi kandamizi, ambazo zimekuwa kikwazo katika kumaliza tatizo la mimba na ndoa za utotoni.


Amezitaja kata hizo kuwa ni Ulowa, Ushetu, Ukune, Kisuke, Uyogo,Kimampula, Bulungwa, na Ulewe, kwa kutoa elimu mbalimbali ambazo zinahusu malezi bora kwa watoto, kwa kushiriki wazazi wa pande zote mbili baba na mama na siyo kumwachia mzazi mmoja, likiwamo pia na suala la kutokomeza mila na desturi kandamizi.


Kwa upande wake, Mratibu wa mradi huo wa kupinga mila na desturi kandamizi kutoka Shirika la KIWOHEDE Victor Reveta, ambao ndiyo wanatekeleza mradi huo kwenye kata nane za halmashauri ya Ushetu, amesema ulianza mwaka 2017 na unatarajiwa kukoma mwaka huu 2019, ambapo pia wamewajengea uwezo wanaume 25 kwa ajili ya kuendelea kutoa elimu kwa wanaume wenzao dhidi ya kutokomeza tamaduni hizo ambazo zimeshapitwa na wakati.

Afisa Maendeleo wa halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama Aminael John akizungumza kwenye Tamasha la Mwanaume Jasiri la Kupinga Mila na Desturi Kandamizi ambazo zimekuwa zikichangia mimba na ndoa za utotoni kuendelea kuwepo kwenye kata ya Ulowa na kuwaasa wanaume waachane na mila hizo. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Kaimu Mkurugenzi kutoka shirika la Save The Children mkoani Shinyanga Alex Enock akielezea malengo ya mradi huo wa kutokomeza mila na desturi kandamizi kwenye halmashauri hiyo ya Ushetu wilayani Kahama, kuwa ni kutokomeza tatizo la mimba na ndoa za utotoni.

Mratibu wa Mradi wa Kutokomeza Mila na Desturi Kandamizi kutoka Shirika la KIWOHEDE wilayani Kahama Victor Reveta akielezea namna wanavyoutekeleza mradi huo katika halmashauri ya Ushetu katika kata nane, kuwa ni utoaji wa elimu wa kupinga mila hizo, elimu ya malezi pamoja na kuunda vikundi vya Wanaume Jasiri ambao watakuwa mabalozi wa kutoa elimu ya kutokomeza mila kwa wanaume wenzao.

Lenard Mboje akisoma risala kwa niaba ya Wanaume Jasiri 25 ambao wamejengewa uwezo wa kutoa elimu ya kupinga mila na desturi kandamizi kwa wanaume wenzao ,amebainisha kuwa kwa sasa kumeibuka mbinu mpya ya kuozesha wanafunzi ndoa za utotoni kwa kuweka ma Bibi harusi bandia ambao wemetimiza umri wa miaka 18, lakini kumbe muolewaji ni chini ya umri huo.

Wananchi wakiendelea kusikiliza elimu ya kupinga mila na desturi kandamizi ili kutokomeza mimba na ndoa za utotoni na kuweza kutimiza ndoto za mtoto wa kike kielimu.

Wananchi wakiendelea kusikiliza elimu ya kupinga mila na desturi Kandamizi, ili kumuokoa mtoto wa kike kielimu kwa kutokomeza tatizo la mimba na ndoa za utotoni.

Burudani ya uvutaji kamba ikitolewa kwenye tamasha hilo la mwanaume jasiri la kupinga mila na desturi kandamizi ili kutokomeza tatizo la mimba na ndoa za utotoni.

Burudani ikiendelea kutolewa kwenye Tamasha hilo kwa kukimbia mbio za kwenye magunia.

Burudani ya kukimbia mbio na mayai nayo ikitolewa kwenye Tamasha hilo la Mwanaume Jasiri katika kata ya Ulowa.

Mchezo wa kukimbiza kuku nao ulikuwepo ambao washindi walipewa zawadi zao.

Mchezo wa kukimbiza kuku ukiendelea.

Wasanii nao walikuwepo kwenye Tamasha hilo la Mwanaume Jasiri la kupinga mila na desrturi Kandamizi, ili kutokomeza mimba na ndoa za utotoni.

Washindi walioshiriki michezo mbalimbali kwenye Tamasha hilo la Mwanaume Jasiri wakiondoka na zawadi zao.

Washindi walioshiriki michezo mbalimbali kwenye Tamasha hilo la Mwanaume Jasiri wakiondoka na zawadi zao.