NA MWAMVUA MWINYI, CHALINZE
MBUNGE wa jimbo la chalinze wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani ,Ridhiwani Kikwete amekabidhi msikiti wa Masjid Swafiya uliojengwa kwa msaada wake kwa kushirikiana na Taasisi ya Miraji Islamic Center.

Akizungumza wakati akikabidhi msikiti huo, kata ya Pera kitongoji cha Magome ,aliwataka waislamu ,kutumia nafasi ya kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kuiombea serikali pamoja na kuwaombea viongozi mbalimbali ili waendelee kuwaletea maendeleo.

Aidha mbunge huyo alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ,kwa juhudi zake anazozifanya katika utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) kwa ufanikishaji wa maendeleo kwa wananchi wanyonge na kuinua uchumi.

Hata hivyo ,Kikwete alisisitiza ,mwezi huu wa Ramadhani ni mwezi ambao tunasisitizwa kusoma Qur'an kwasababu mwezi huu wa Ramadhan ndio Qur'an ilimshukia Mtume ili uwe muongozo kwa watu hapa duniani, pia usomaji huo unamalipo makubwa kwa Mungu.

"Kipindi kama hiki cha mfungo tunatakiwa kumcha mungu na kusaidia masikini kwani funga inamaana kubwa sana ,hivyo kila muislamu aliyefanikiwa kupata nafasi hapa duniani ni lazima amsaidie mwenzake japo futali"alisema Kikwete.

Nae Shekhe Mohammed ,alimpongeza mbunge huyo kwa kutambua thamani ya uislamu na hata kujitolea kwa ari na mali katika ufanikishaji wa ujenzi wa msikiti huo .

Hivyo anamwakikishia Kikwete kuwa wao kama viongozi wa dini wataendelea kuliombea Taifa ili liondokane na majanga ya aina yeyote