RAIS wa zamani wa Argentina, Cristina Fernandez de Kirchner, amefunguliwa mashitaka ya rushwa, tukio lililokuja siku tatu baada ya kutangaza kwake kuwania nafasi ya makamu wa rais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Kirchner anatuhumiwa kumpendelea mfanyabiashara Lazaro Baez ili kupatiwa zabuni za umma zenye thamani ya mamilioni ya dola wakati akiwa rais mwaka 2007 – 2015.
Mfanyabiashara huyo anayetokea jimbo la Santa Cruz ambako ni ngome ya Kirchner, anahisiwa kuanza kupata upendeleo wa aina hiyo wakati Nestor Kirchner ambaye ni mume wa Cristina alipokuwa rais kati ya mwaka 2003 hadi 2007.
Sambamba na hayo Kirchner pia anakabiliwa na madai ya ufisadi, lakini madai hayo bado hayajafikishwa mahakamani.