Rais Magufuli Mbele ya Rais wa Zimbabwe “Mna Upungufu wa Mahindi Nitawauzia”
Jana May 29, 2019 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema Tanzania itaiuzia Zimbabwe tani 700,000 za mahindi kufuatia nchi hiyo kukabiliwa na upungufu wa chakula.

Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo leo muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo rasmi kati yake na Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa yaliyofanyika Ikulu Jijini Harare.

Ameeleza kuwa katika msimu uliopita Tanzania ilipata ziada ya chakula ya tani Milioni 3.3 baada ya kuvuna tani Milioni 16.8 ambapo kati yake mahitaji ya nchi ni tani Milioni 13.5.

Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli ameikaribisha Zimbabwe kujifunza jinsi Tanzania inavyotoa mafunzo ya kujenga Taifa kwa vijana kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na amebainisha kuwa JKT inasaidia vijana kuwa wazalendo wa kweli, kuwa na nidhamu na wakakamavu.

Rais Magufuli pia ameelezea kutofurahishwa kwake na kutofanyika kwa Kamati ya Kudumu ya Pamoja (Joint Permanent Commission – JPC) tangu mwaka 1998 hali iliyosababisha kukosekana kwa msukumo wa kutosha wa kutekeleza maeneo muhimu ya uhusiano yenye kuimarisha uchumi wa pande zote na hivyo ametaka Mawaziri na Wataalamu kufanya kikao cha JPC ndani ya mwezi mmoja.

Aidha, Rais Magufuli amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa rafiki wa kweli wa Zimbabwe na ameahidi kuwa tayari kuwaleta walimu watakaofundisha lugha ya Kiswahili katika shule na vyuo vya Zimbabwe.