Mabingwa wa Ufaransa Paris Saint Germain wametangaza kuwa kufuatia staa wao wa kimataifa wa Brazil Neymar kutangaza kuadhibiwa kwa kufungiwa mechi tatu, wao hawakubaliani na hilo hivyo baada ya kukaa chini na kujadili watakata rufaa kuhusiana na adhabu hiyo.

Neymar aliingia matatizoni mwezi uliopita baada ya kusambaa mtandaoni video yake akimsukuma shabiki baada ya PSG kufungwa katika mchezo wa fainali ya Copa De France, hivyo baada ya kusambaa kwa video hiyo chama cha soka Ufaransa FFF ikatangaza kumuadhibu kwa kumfungia mechi tatu.Taarifa kutoka PSG zinaelezwa kuwa wanakata rufaa kuhusiana na adhabu hiyo kutokana na shabiki yule, aliwatukana baadhi ya wachezaji wa PSG akiwemo Neymar ambaye alikasirishwa na kumsukuma, hivyo hawaoni kama Neymar alistahili adhabu hiyo, katika mchezo huo wa fainali ya Copa de France dhidi ya Rennes ilimalizika kwa sare ya kufungana 2-2 ila penati Rennes wakashinda 9-8.