KATIBU Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome amekutana na watoa huduma ya msaada wa kisheria jijini Arusha na kuwataka kuleta matokeo kupitia huduma ya msaada wa kisheria.
Prof Mchome alikutana na watoa huduma ya msaada wa kisheria jijini Arusha ikiwa ni sehemu ya ziara ya ukaguzi wa shughuli za msaada wa kisheria zinazotolewa kwa wananchi ili kuboresha huduma hizo kwa wananchi.
“Msaada wa kisheria unalenga kumsaidia mwananchi ilia pate matokeo fulani, nakama mkishindwa kupata matokeo mtakuwa hamjatimiza lengo la kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa Kisheria,” amesema Prof. Mchome.
Amesema Sheria ya Msaada wa Kisheria No.1 ya 2017 imelenga kupata matokeo kama ya kusaidia mwananchi-1 kupata haki yake na kama kumaliza kesi bila ya kuzipeleka Mahakamani basi hayo ni matokeo chanya kwani inawezesha Serikali na mwananchi husika kuokoa fedha ambazo zingetumika kufungua na kuendesha kesi kutumika kwa shughuli nyingine za maendeleo.
Prof. Mchome pia amewataka watoa huduma hao kupitia wasaidizi wa sheria kuhakikisha huduma ya msaada wa kisheria inatolewa kwa wananchi wenye uhitaji ambao wanakidhi vigezo ambavyo vipo kwa mujibu wa sheria.
Amesema sheria ni chombo cha maendeleo na zinakuwepo ili kutengeneza njia sahihi ili wananchi kupita na hivyo kupata haki zao na maendeleo kwa ujumla.
“Sheria zipo ili kuleta aina fulani ya utaratibu na maendeleo ya nchi, sio wote wanayajua hayo, sheria inafanya kazi hiyo inakuelekeza kwa kuanzia na msaada wa kisheria ni pamoja na kufanya kazi ya kuelekeza njia ya kufuata kupata haki na kutatua kero ya wananchi,” alisema.
Wizara ya Katiba na Sheria iko katika ziara ya kuwatembelea watoa huduma za msaada wa kisheria nchini kwa ajili ya kukagua wanavyotoa huduma zao na kujua changamaoto zinazowakabili ili kuboresha huduma za msaada wa kisheria nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watoa huduma ya msaada wa sheria kwa wananchi jijini Arusha