Katibu Mkuu Wizara ya Maji Prof. Kitila Mkumbo (kushoto) akisaini Mkataba wa mradi wa maji katika miji 29, kulia, ni Meneja Mkazi wa kampuni ya WAPCOS kutoka India. Bw. Chandrasekhal Kombathula. Kampuni ya WAPCOS imepewa muda wa miezi miwili kumaliza kazi ya awali ili Wakandarasi wawepo katika eneo la mradi kuanza kazi. Mradi huo wenye thamanani ya Dola za Marekani milioni 500.

Wizara ya Maji imesaini mkataba wenye thamani ya Shilingi Bilioni 15.6 na Kampuni ya WAPCOS kutoka India ili kuanza kutekeleza mradi wa maji wa miji 29.

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo, pamoja na Meneja Mkazi wa Kampuni ya WAPCOS Ltd, Bw. Chandrasekhar Kombathula wamesaini mkataba huo, wenye sehemu mbili, jijini Dodoma.

Profesa Mkumbo akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini amesema kazi hiyo inafanyika ukiwa ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim ya India wenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani milioni 500.

Amesema mkataba uliosainiwa leo ni hatua ya awali na unahusu kazi mbili (lots) ambazo ni kuandaa taarifa ya kina kuhusu miradi yote wa miji 29 (detailed design) ikiwemo maeneo maji yatakapopatikana na ya pili ikiwa kuandaa nyaraka za zabuni ili kuwapata Wakandarasi watakaotekeleza mradi.

 Kampuni ya WAPCOS imetakiwa kumaliza kazi hiyo ndani ya kipindi cha miezi miwili baada ya kusaini mkataba huo leo. Wakandarasi wa kutekeleza mradi wanatakiwa wawe eneo la kazi ifikapo Septemba 2019. Mradi wa maji wa miji 29 unatarajia kuhudumia zaidi ya wananchi milioni mbili.
                                    
Imetolewa na
 Kitengo cha Mawasiliano 
14 Mei, 2019