Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam mnamo tarehe 25/05/ 2019 majira ya saa nane usiku huko maeneo ya Kigogo Fresh Mtaa wa Seremala lilifanikiwa kuwaua majambazi watatu akiwemo mwanamke mmoja na kisha kukamata bastola mbili aina ya Browning zilizofutwa namba na risasi tatu .

Awali jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam lilipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna kikundi cha majambazi wapatao watano wamepanga kuvamia nyumba ya Bwana ALLY DASTAN (66), Mkazi wa Kigogo Fresh ambaye mke wake aitwaye MOSHI SAID(56) ni Mwenyekiti na ni mtunza hazina  wa Kikundi cha Umoja Group.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kupitia kikosi kazi Maalum cha kupambana na ujambazi kiliweka mtego katika nyumba  ya Bwana ALLY na ilipofika majira ya saa nane usiku majambazi hao wapatao watano walivamia nyumba hiyo na baada ya kugundua kuwa kuna mtego wa polisi walianza kurusha risasi na ndipo askari wakajibu mapigo na kufanikiwa kuwajerui majambazi watatu akiwemo mwanamke mmoja na majambazi wawili walikimbia. Majambazi hao walifariki dunia wakiwa njiani wakipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linaendelea kuwasaka majambazi wawili waliokimbia.