Na Editha Karlo wa Michuzi TV, Uvinza.
MKUU wa wilaya ya Uvinza Mwanamvua Hoza, amewataka wakulima wadogo wadogo kuchangamkia fursa ya kujiunga na mfuko wa fao la ushirika afya kutoka mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF), kwani wametambua umuhimu wa uwepo wao katika vyama vya ushirika.
Akizungumza leo na wakulima wa zao la tumbaku katika kijiji cha Basanza wilayani uvinza mkoani Kigoma Mwamvua zao la tumbaku ni moja ya zao la kimkakati nchini na kwamba ni muhimu kuliboresha pamoja na wakulima wake.
" Nichukue fursa hii kuwahamasisha wakulima kujiunga na mfuko huo kwani ugonjwa ukija hautoi taarifa ni muhimu kila mmoja wetu akawa na kadi ya bima ya afya yeye na familia yake," amesema Hoza.
Aidha Mkuu wa wilaya huyo amewataka wananchi kuuza mazao yao baada ya kuvuna na kuhakikisha wanaweka na akiba ya chakula Kwani serikali haitampatia mtu chakula kwa kufanya uzembe kama huo.
Mkulima Mwajabu Hassan ameiyomba serikali kupitia mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF), kupunguza kiwango cha fedha cha kulipia katika mfuko huo.
"Tunaomba serikali yetu kutusikia sisi wanakijiji cha Basanza wakapunguza kiwango kutoka Sh 76,800 hadi Sh 38,400 ili kila mmoja aweze kupata matibabu, "amesema Hassan.
Mkulima wa tumbaku Beatrice Musule amesema, amesema wakulima hawawezi kumudu gharama hizo kutokana na wakati mwingine wanakosa mavuno kwasababu ya wadudu wanaoharibu mazao yao.
"Afya ni jambo nzuri na wametuletea wakati mzuri lakini tunaomba serikali yetu sikivu ituangalie sisi wakulima wadogo wa tumbaku iweze kupunguza kiwango ili tuingie na familia zetu," amesema Masule.
Naye Michael Stephano amesema ni vema wakaliangalia jambo hili kwa mara ya pili na kuwaruhusu kulipia taratibu kwa awamu nne kutokana na umuhimu wa jambo la afya.
" Tutalipa kiasi hicho lakini tunaomba watuwekee utaratibu wa kulipa kwa awamu au watupunguzie kiwango kila mmoja anatamani kujiunga lakini tunashindwa," amesema Stephano.
Meneja wa NHIF mkoa wa Kigoma Benard Katerengabo, amesema wataendelea kutoa elimu kwa wakulima na vyama vya ushirika mkoani humo lengo likiwa ni kila mkulima aweze kunufaika na matibabu yeye pamoja na familia yake.
Amesema baada ya kuwapa elimu wanaushirika wa vyama vya ushirika Basanza, wametoa maoni yao pamoja na kukatwa kiasi hicho cha fedha kwa wanachama wakati wa kipindi cha mavuno kwa kutambua umuhimu wa matibabu.
Meneja wa mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF), mkoani Kigoma Benard Katerengabo akizungumza na wakulima wa zao la tumbaku katika kijiji cha Basanza wilayani Uvinza(hawapo pichani) akitoa elimu kuhusiana na kujiunga na mfuko wa fao la ushirika afya.
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mwanamvua Mrindoko akiwahamasisha wakulima wa zao la tumbaku katika kijiji cha Basanza kujiunga na fao la ushirika la afya ili kuwa na uhakika wa matibabu pale wanapougua wao pamoja na familia zao.
Baadhi ya wakulima wa zao la Tumbaku katika kijiji cha Basanza Wilayani Uvinza wakisikiliza elimu ya kujiunga na fao la ushirika kupitia mfuko wa bima ya afya Taifa(NHIF)