Na Subira Kaswaga (Afisa Habari NEC)

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza tarehe 15, Juni mwaka huu kuwa ni siku ya kufanyika kwa Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata 32 zilizopo katika halmashauri ishirini (20) za Tanzania Bara.

Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam Makamu, Mwenyekiti wa NEC Jaji (R) Mbarouk S. Mbarouk amesema kuwa, Tume imetangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya serikali za Mitaa, juu ya uwepo wazi wa nafasi 31 za Udiwani katika Kata 31 za Tanzania Bara kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kujiuzulu na vifo.

Aidha, amesema kuwa, Tume imetangaza kufanyika kwa Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata ya Kitangiri Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza sambamba na kata hizo 31, baada ya Mahakama ya Rufaa kuondoa maombi ya mapitio yaliyowasilishwa katika Mahakama hiyo, kufuatia kutenguliwa kwa matokeo ya Uchaguzi wa Udiwani katika kata hiyo.

Jaji (R) Mbarouk amesema kuwa, fomu za uteuzi wa Wagombea zitatolewa kati ya tarehe 27 hadi 31 Mei, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 31 Mei, kampeni za uchaguzi zitaanza tarehe 01 Juni hadi 14 Juni mwaka huu na tarehe 15 Juni, mwaka huu ndiyo itakuwa siku ya uchaguzi.

Amezitaja kata zitakazofanya uchaguzi huo kuwa ni Mto wa Mbu, Mkuyuni na Majengo zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Kata za Ganako, Daa, Mbulumbulu, Oldeani na Kanssay zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha. Kata ya Likuyuseka iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Kata za Kinyasiti kati iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na Kata ya Kikombo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma mkoani Dodoma, Kata ya Itenka iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi, Kata za Ipole na Pangale zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge na Kata ya Itumba iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Igunga za mkoani Tabora.

Nyingine ni Kata ya Boma iliyopo Halmashauri ya Mji wa Mafinga mkoani Iringa, Kata za Tandika na Chikongola zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara, Katika Mkoa wa Dar es Salaam zip Kata za Bonyokwa iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Kata ya Tungi iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni na Kata ya Chang’ombe iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.

Pia Kata ya Ruangwa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Kata za Mkula na Lamadi zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, Kata za Kibosho Magharibi na Uru Shimbwe zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi za mkoani Kilimanjaro, Kata ya Murangi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoa wa Mara na Kata ya Siuyu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Pamoja na Kata za Kyaitoke, Mugajale na Ruhunga zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera na Kata ya Kitangiri iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imevikumbusha vyma vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya Uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume wakati wote wa kipindi cha Uchaguzi huu mdogo.