Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekana kuhusika na matangazo ya kihalifu ya ajira yaliyosambazwa maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia, NEC ameutaarifu umma kuwa haihusiki na matangazo hayo yenye lengo la kuwatapeli wananchi kuwa, Tume imetoa ajira za muda.

Dkt. Kihamia alifafanua kuwa kutokana na tangazo hilo, wananchi walioomba ajira hizo wamekuwa wakiambiwa watoe kiasi cha fedha kwa madai kuwa ni kwa ajili ya mafunzo.

“Hatua kali za Kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu au kundi la watu wanaotumia au wanaopanga kutumia jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya vitendo vya kihalifu” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika taarifa yake, Dkt. Kihamia aliwasihi wananchi kuendelea kutoa taarifa mara tu wanapohisi uwepo wa watu au kundi la watu wenye nia mbaya ya kulichafua jina la Tume yaTaifa yaUchaguzi.