Robert Marawa amethibitisha taarifa hizo kupitia ukarasa wake wa Twitter kwa kueleza kuwa alitumiwa ujumbe mfupi na Mabosi wake kuwa asifike ofisini kwenye kipindi cha TNL kwani mkataba wake umeisha.

Kufuatia tukio hilo, Supersport wametoa tangazo kuwa wanatarajia kufanya mabadiliko ya watangazaji wa ndani kwa kuangalia  upya marekebisho ya baadhi ya mikataba ikiwemo wa Robert Marawa.Duru za habari nchini Afrika Kusini, zinaeleza kuwa Mtangazaji huyo kupitia ukurasa wake wa Twitter siku tatu zilizopita aliandika ujumbe ulioashiria kuwa kuna baadhi ya makampuni makubwa yanawalipa watu wanaofanya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

Robert Marawa ni moja ya watangazaji wa michezo wanaovutia zaidi kuwasikiliza, hususani kwa wale watu wanaofuatilia michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya na Kombe la Mataifa huru Afrika.

Ameshawahi pia kutangaza kipindi cha Sports Zone cha Shirika la Habari Afrika Kusini (SABC) na baadae alifukuzwa kisha akajiunga na SuperSport.

Hatua hiyo ya kufukuzwa kwake imepokelewa na baadhi ya mashabiki kama’ ushujaa’ kwani ameongea vitu ambavyo anaona haviko sawa.