DAR ES SALAM: Dansa maarufu anayeitumikia Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Moses Iyobo ‘Moze’, anadaiwa kuingia mitini kuhudhuria birthday ya mwanaye, Cookie aliyezaa na mwigizaji Aunt Ezekiel.Shughuli hiyo ilifanyika nyumbani kwa Aunt maeneo ya Victoria jijini Dar, juzi na kuhudhuriwa na watu mbalimbali. Akizungumza na Gazeti la Ijumaa, Aunt ambaye aliandaa futari kwenye kumbukizi hiyo ya kutimiza miaka minne ya Cookie alisema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwani siku hiyo ilifana.


Aunt alisema alichokuwa anakitaka kwa mwanaye ni kufurahi, jambo ambalo alilitimiza na kutoa sadaka yake ya futari kwa watu waliohudhuria.

“Kikubwa nilichokuwa ninakitaka ni mwanangu awe na furaha na kutimiza sadaka kwa mtoto wangu kwa kuwafuturisha ndugu, jamaa na marafiki na hilo Mungu amelifanikisha na kama kuna jambo lingine halikwenda sawa, litakamilika tu bila shaka,” alisema Aunt.


Akizungumzia ishu ya Iyobo kutofika kwenye birthday ya mtoto wake, Aunt alisema hajui labda kuna kitu kimempata, lakini kama ni mwaliko alipewa kwa vile yeye ni baba mtoto.

“Nilimwalika, si ni baba mtoto? Sasa nitaachaje kumwambia ishu ya mwanaye? Labda kuna kitu kilimtinga hivyo akashindwa kufika,” alisema Aunt. Sherehe hiyo ilifana kwa sababu kila aliyehudhuria alivaa kistaarabu na kila mmoja alikula na kunywa hadi kusaza.

Gazeti la Ijumaa lilimtafuta Iyobo kwa njia ya simu ambapo iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi, hakujibu. Hivi karibuni uhusiano wa Aunt na Iyobo ulivunjika rasmi baada ya tetesi za muda mrefu ambapo sasa kila mmoja anaishi kivyake huku mtoto akibaki kwa mama yake.