Kwa mara ya kwanza wachezaji watatu kutoka barani Afrika wameshinda tuzo ya ufungaji bora kwenye Ligi Kuu ya England EPL kwa mkupuo baada ya wote kuhitimisha msimu hii leo wakiwa na mabao 22 kila mmoja.

Wachezaji hao ni Mohamed Salah wa Liverpool anayetoka nchini Misri, Sadio Mane wa Liverpool kutoka nchini Senegal na Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal ambaye ni raia wa Gabon.

Wachezaji wote watatu wamekabidhiwa tuzo zao leo katika michezo ya mwisho ya ligi hiyo, iliyomalizika kwa Manchester City kutetea ubingwa wao kwa kifikisha pointi 98 na Liverpool kumaliza wakiwa nafasi ya pili na pointi 97.

Kabla ya mechi za leo, Salah alikuwa akiongoza kwa tofauti ya magoli mawili kati yake na wenzake, lakini katika mechi za leo, Aubameyang amefunga mabao mawili kwenye ushindi wa 3-1 wa Arsenal dhidi ya Burnley huku Mane naye akiifungia mabao yote mawili Liverpool ikishinda 2-0 dhidi ya Wolves.

Huu ni msimu wa pili mfululizo kwa Salah kushinda tuzo hiyo baada ya msimu uliopita kuibuka kinara akifunga mabao 32, hivyo amefikia rekodi ya Harry Kane, Thiery Henry, Alan Shearer, Michael Owen na Robin Van Parsie kushinda tuzo hiyo mara mbili mfululizo.