MWEKEZAJI wa Simba, bilionea, Mohamed Dewji ‘Mo’ ameahidi kuwapa bonsai ya shilingi milioni tano wachezaji wa timu hiyo wagawane kwa kila mechi watakayoshinda kati ya mechi nne walizobakiza, ikiwemo ya jana dhidi ya Ndanda.



Mo alitangaza neema hiyo, Ijumaa iliyopita mara baada ya kukutana na wachezaji, Benchi la Ufundi la timu hiyo na kula futari kwa pamoja kwenye moja ya hoteli kubwa jijini Dar es Salaam.



Kwa mujibu wa taarifa ambazo limezipata Championi Jumatatu, wachezaji hao watapewa bonsai hiyo kwenye michezo minne waliyoibakisha ya ligi ukiwemo wa jana walipocheza dhidi ya Ndanda FC.



Mo ameongeza dau hilo, ukiachana na Sh 400,000 ambazo amekuwa akitoa kwa kila mchezaji kila wanaposhinda, tangu ligi imeanza.



Mtoa taarifa huyo alisema, Mo amewaongezea bonasi hiyo kwa ajili ya kuwaongezea morali na hamasa ili wafanikishe malengo ya kutwaa ubingwa.


Aliongeza kuwa, Mo anataka kuona timu yake inashinda michezo yote minne waliyoibakisha na lengo ni kuchukua ubingwa mapema kabla ya michezo ya ligi kumalizika.



“Mo alikutana na kuzungumza mengi katika kikao chake allichokiitisha kati yake, Benchi la Ufundi la Simba na wachezaji wake na katika kikao hicho mengi yalizungumzwa.



“Kati ya hayo mengi ni kuwaongezea morali na hamasa ya timu katika kuelekea michezo minne waliyoibakisha na zaidi kuwapa bonsai ya Sh Mil 5 wachezaji pale timu ikipata ushindi katika michezo yao ya ligi, hii ni tofauti na shilingi 400,000 waliyokuwa wanapewa kila mchezaji katika michezo iliyopita timu ikiwa napata ushindi.



“Bonasi hiyo itatolewa mara baada ya mechi kumalizika ya ligi, Mo anataka kuona timu inashiriki tena Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara mbili mfululizo na ndiyo sababu ametoa ahadi ya kuwapa bonasi hiyo,” alisema mtoa taarifa huyo.





Alipotafutwa mwenyekiti wa timu hiyo, Swedy Mkwabi kuzungumzia hilo alisema: “Ni kweli Mo alikutana na benchi la ufundi na viongozi na mengi yalizungumzwa na kati ya hayo ni siri ya timu, hivyo siwezi kuweka wazi kwani nitakuwa naweka wazi mipango ya timu.”