Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya awamu ya nne, Bernard Membe amemjibu mfanyabishara Rostam Aziz kuhusu suala la kugombea urais 2020 akimtaka hivi sasa ajikite kwenye masuala ya kitaifa yanayohusu uchumi.

Membe ametoa kauli hiyo akiwa nje ya jengo la Mahakama kuu ya Tanzania, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka kusikilizwa kwa kesi anayodai fidia dhidi ya mmiliki wa gazeti la Tanzanite Cyprian Musiba, ambapo aliulizwa swali kuhusiana na kauli inayodaiwa kutolewa na mfanyabiashara Rostam Aziz kuhusiana na uchaguzi wa mwakani.

Jana Mei 16, 2019, picha moja ya video ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Rostam akizungumzia suala la urais 2020 na kumshauri Membe asijitokeze kuwania nafasi hiyo badala yake aachiwe Rais John Magufuli kwa awamu nyingine.

Membe amesema kuwa ; "Kuhusu kugombea mwakani napata kigugumizi kumjibu Rostam, lakini yeye ni mchumi na nitakutana naye nimshauri anafanya vizuri kwa Watanzania anapozungumzia masuala ya uchumi, inabidi azungumzie 'main issue' za nchi sio 'personal', hizi tunaachia watu wa chini."

"Kwa 'level' yetu ni kuzungumzia masuala ya kitaifa masuala ya kiuchumi, kwanini uchumi wetu upo hapa ulipo? kwanini wafanyabiashara wanafunga biashara zao, Rostam ni 'economist' namshauri ajiadress kwenye masuala ya kiuchumi, Rostam wewe ni mwenzetu sisi tumekatwa mkia." amesema Membe.

"Ukikatwa mkia hata ujitahidi vipi mkia wako ni mfupi tu, tunayoyazungumza ni vizuri tuwe 'consistency' mdomoni na dhamira yetu, Rostam ni mchumi mzuri sana, tuzungumzie masuala ya uchumi wa nchi yetu, kuliko kujaribu kuwa mtoto mzawa badala ya kukubali 'status' ..Rostam na mimi ni watoto wa kambo." alimalizia Membe.