Mbunge wa Segerea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bonnah Kaluwa ametoa taarifa ya kubadilisha jina kufuatia kuingia kwenye mvutano wa matumizi ya jina na mume wake Moses Kaluwa ambapo sasa atafahamika kwa jina la Bonnah Kimoli.

Uamuzi wa Mbunge huyo wa Segerea umetangazwa leo Mei 16,2019 Bungeni jijini Dodoma kupitia Spika wa Bunge, Job Ndugai ambapo amesema ameeleza kupata taarifa kutoka kwa mbunge huyo.

“Nimetaarifiwa kuwa Mheshimiwa Bonnah amebadili jina na sasa anatumia jina la Bonnah Ladislaus Kamoli”, amesema Spika Ndugai.

April 28, 2019 kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mbunge huyo wa Segerea  aliandika ujumbe kwamba tuhuma ambazo zilikuwa zikisambaa kwenye mtandao wa kijamii kuwa alifumaniwa na mumewe hazikuwa na ukweli.

"Wahenga wanasema jambo likiongelewa sana bila majibu linaweza kugeuka likawa kweli. Sasa ni hivi mimi Bonnah Ladislaus Kamoli au jina langu lingine Neema, sijawahi kufumaniwa hata siku moja katika maisha yangu". aliandika Bonnah

"Sio kwamba mimi ni muadilifu sana au malaika ila hapakuwepo na mtu wa kunifumania nadhani mtakua mmenielewa na sitaongea tena na kama kuna mtu ana ushahidi alete na kanifumania na nani", alimaliza Bonnah katika maelezo yake.