MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Ruvuma Dk.Abdulla Juma Mabodi ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Songea Vijijini kuharakisha Uchunguzi wa Matumizi ya Fedha ya Shilingi Milioni 10 zinazosadikiwa kutumiwa vibaya katika Ujenzi wa Kituo Cha Afya cha Kijiji Cha Mpangula Kata ya Matimila. 

Fedha hizo zilikuwa za kumalizia Matengenezo ya mwisho ya Kituo hicho kwa kupiga Plasta,Sakafu,milango na Jipsomu na zikaisha bila Jengo hilo kukamilika.   

Agizo hilo amelitoa katika mwendelezo wa ziara yake Mkoani humo katika Wilaya ya Songea Vijijini wakati akikagua Ujenzi wa Kituo hicho kilichojengwa kwa Michango ya Wananchi kwa Kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya  pamoja na Fedha za Mfuko wa  Jimbo la Peramiho chini ya Mbunge wake Mhe. Jenista Mhagama. 

Aliisisitiza TAKUKURU kukamilisha Uchunguzi huo kwa haraka ili kupisha shughuli zingine ziendelee kwa lengo la kukamilisha  Ujeni wa Kituo hicho na Wananchi wapate huduma za Afya.  

Alisema Wananchi wa Kijiji hicho na maeneo jirani wanahitaji huduma bora za Afya kutoka katika Kituo hicho ambacho fedha nyingi zilizotumika imetokana michango inayotokana na nguvu zao. 

 Dk.Mabodi ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, aliwataka Watendaji wa Serikali wanaohusika na kusimamia Miradi mbali mbali ya Maendeleo zikiwemo Ujenzi wa Nyumba za Umma kuacha Tabia za kukaa Ofisini badala yake waende katika maeneo husika kusimamia ujenzi ili kuepuka matumizi mabaya ya Fedha za Umma. 

“Nawasisitiza Watendaji Wote wanaosimamia utekelezaji wa miradi ya Serikali kushuka kwa Wananchi kwa lengo la kusimamia ipasavyo miradi ya Serikali kwani msipofanya hivyo kuna baadhi ya Watu wanatumia nafasi hiyo kujinufaisha wenyewe na kusababisha miradi kukwama.”,alisema Dk.Mabodi. 

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma,Oddo Kilian Mwisho alisema Serikali Kuu kupitia Serikali za Mitaa imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya miradi ya kuimarisha huduma za kijamii ikiwa ni sehemu ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM ili kutatua changamoto za Wananchi. 

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Matimila Menasi Komba amekiri kuwepo kwa changamoto ya matumizi mabaya ya fedha hizo hata hivyo wanahitaji zaidi ya shilingi miilioni sita kukamilisha kazi ili huduma ianze. 

Akizungumza katika Kituo cha Afya cha Mpangula Dk.Mabodi alishiriki Ujenzi wa Taifa wa kujenga Kituo hicho kinachotarajiwa kuhudumia zaidi ya Watu 20,000.   

Sambamba na hayo Dk.Mabodi alizungumza na Wana CCM wa Shina no. 1 Tawi la CCM Muhungu Kata ya Matimila Wilaya ya Songea Vijijini, na kuwaeleza kwamba Siasa ya Ujamaa iliyoasisiwa na Vyama vya Ukombozi vya ASP na TANU vilianzisha Mfumo wa Mashina kwa nia ya kujiweka karibu na Wananchi. 

Awali mara baada ya kuwasili katika Tawi hilo Dk.Mabodi alipokelewa na Wazee wa CCM wa Kijiji hicho na kumtunuku Heshima ya Uchifu wa Kingoni wenye Asili ya Chifu wa Songea Mbano kwa kumkabidhi Ngao,Mkuki na Kinjenje kwa ajili ya kujikinga na Maadui wa kuihujumu CCM. 

Katika ziara yake hiyo Dk.Mabodi alikagua Kituo cha Afya cha Mtyangimbole na kusisitiza kuwa ujenzi huo ukamilike kwa wakati ili wananchi wa eneo hilo waondokane na changamoto ya ukosefu wa huduma za Afya. 

Akizungumza na Wanachama wa CCM wa Shina namba Nane (8) Tawi la CCM Mtyangimbole Jimbo la Madaba Wilaya ya Songea Vijijni, aliwataka Wananchi kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura ili wapate haki ya Kuchagua na kuchaguliwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu Ujao. 
 MLEZI wa CCM Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Dk.Abdulla Juma Mabodi akiwa amebeba Ndoo yenye Udongo wa kujengea Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mpangula. 
WAZEE wa CCM wa Kijiji cha  Muhungu wakimpa Dk.Mabodi Heshima ya Uchifu wa Kingoni wenye Asili ya Chifu wa Songea Mbano kwa kumkabidhi Ngao,Mkuki na Kinjenje kwa ajili ya kujikinga na Maadui wa kuihujumu CCM.

 MLEZI wa CCM Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Dk.Abdulla Juma Mabodi (kulia),Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Killian Mwisho(kushoto) wakipanda Mti katika Kituo cha Afya Mtyangimbole. 
MLEZI wa CCM Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Dk.Abdulla Juma Mabodi na akizungumza na Wananchi na Wanachama wa CCM wa Shina namba Nane (8) Tawi la CCM Mtyangimbole Jimbo la Madaba Wilaya ya Songea Vijijni.