Serikali ya Marekani imeondoa kwa muda vikwazo vya kibiashara ilivyoweka wiki iliyopita dhidi ya kampuni ya simu ya China Huawei, hatua inayolenga kupunguza hali ya kuvurugwa wateja wake.

Hatua hiyo hata hivyo imepuuziliwa mbali na muasisi wa kampuni hiyo anayesema kuwa Huawei ilikuwa imejiandaa kwa hatua ya Marekani.

Wizara ya Biashara ya Marekani itairuhusu kampuni ya Huawei kununua bidhaa zinazotengenezwa Marekani kwa siku nyingine 90 ili kudumisha mitandao iliyopo na kutoa programu tumishi mpya kwa simu za sasa za Huawei.

Kampuni hiyo kubwa kabisa duniani ya kutengeneza vifaa vya mawasiliano ya simu bado imezuiwa kununua vifaa kutoka nchini Marekani vya kutengenezea bidhaa mpya bila idhini za leseni ambazo kuna uwezekano kuwa zitakataliwa.

Serikali ya Marekani ilisema iliweka vikwazo hivyo kwa sababu ya Huawei kujihusisha na shughuli zinazoenda kinyume na usalama wa taifa au maslahi ya sera za kigeni.