MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola  ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu England msimu huu wa 2018/19 amesema kuwa anawashukuru sana wapinzani wake Liverpool kwa namna walivyokuwa wanampa presha ya kupambana kwenye kila mchezo.
Manchester City msimu huu wametwaa kombe wakiwa na tofauti ya pointi moja na wapinzani wao Liverpool ambao wana pointi 97 huku wao wakiwa na jumla ya pointi 98 zilizowapa ubingwa msimu huu.
"Nina kila sababu za kuwashukuru na kuwapongeza Liverpool kwa hakika nina kila sababu za kuwaambia asante tena asante wametusaidia kutwaa ubingwa.
"Msimu uliopita tulifanya vizuri walitusaidia kupambana na kuongeza juhudi zaidi, kushindana na timu inayokushusha na kukupandisha sio jambo la mchezo, ninafurahi kuona nimejikusanyia pointi 198 jumla kwenye misimu miwili.
"Ni kawaida kama utapata pointi 100 inakuwa rahisi kushuka chini, Liverpool wametusaidia kuwa katika hali ya ushindani hivyo ninafurahi kuona tumebaki na kombe msimu huu," amesema Guardiola.