BAADA ya mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo kuonekana akitambulishwa na mabosi wa Klabu ya Horoya AC ya Guinea, Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Mzee Ibrahim Akilimali ameibuka na kusema kuwa amesikitishwa na maamuzi ya mchezaji huyo kuondoka kimyakimya.Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo mwenye mabao 16 katika Ligi Kuu Bara inaelezwa amejiunga na timu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu huku usajili huo ukiwa bado unawashangaza viongozi wa Yanga kwa kudai kutokuwa na taarifa nao.


Mzee Ibrahim Akilimali.

Akizungumza na Championi Jumamosi, mzee Akilimali alisema kuwa, kwa upande wake hadi sasa bado hajajua sababu za mchezaji huyo kuondoka kwa staili hiyo ikiwa bado ana mkataba wa mwaka mmoja na timu yao hali ambayo inamnyima furaha.“Sina raha kabisa nakwambia na wala siamini kwamba Makambo ameondoka Yanga na kwenda kujiunga na timu nyingine, nani amempeleka huko, napata taabu maana sielewi kinachoendelea kwa sababu maumivu ya Kakolanya hayajaisha linakuja hili.“Niwaombe viongozi wetu naamini wana busara kubwa walitafutie ufumbuzi jambo la mchezaji huyo kwa sababu amekuwa msaada mkubwa kwenye timu hasa katika kipindi ambacho tumepitia Yanga na ukiangalia bado tuna mkataba naye wa mwaka mmoja, nadhani cha msingi tusubiri viongozi wetu watuletee majibu,” alisema mzee Akilimali