Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Nicholas William amesema kuwa mafunzo ya ununuzi wa umma kwa Wakuu wa Idara na Vitengo yatasaidia kuondoa utata uliopo kuhusu suala la kusimamia mikataba ya ununuzi wa umma kati ya Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB).

“Kumekua na utata kuhusu suala la yupi mwenye mamlaka ya kusimamia mikataba ya ununuzi wa umma kati ya Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi hivyo natoa rai kwa watoa mafunzo kuondoa utata huo,”alisema Bw. William.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu na yanahitajika hasa kwa viongozi wa umma kwani ndio wahusika wakuu katika kupitisha mikataba mbalimbali ya ununuzi.

Aidha, amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kupunguza muda unaotumika kufanya ukaguzi kwa kuwa mikataba ya ununuzi wa umma haitakuwa na changamoto nyingi kwani wahusika watakuwa na uelewa mpana katika maandalizi ya mikataba hiyo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi, Bw. Godfrey Mbanyi amesema kuwa lengo la kufanya mafunzo hayo ni kuwafanya wanaohusika na kutoa maamuzi juu ya manunuzi ya umma kuwa na uelewa wa pamoja ili kuhakikisha mikataba wanayoingia haileti kasoro yoyote.

“Kumekua na changamoto kwa wakuu hawa wanapoteuliwa kuwa Wajumbe wa Bodi za Zabuni wanakuwa hawajui chochote kuhusu taratibu za ununuzi wa umma hivyo semina hii itawasaidia kufahamu taratibu hizo,” alisema Bw. Mbanyi.

Bw. Mbanyi ameongeza kuwa kutokujua taratibu za manunuzi ya umma zinawasababishia matatizo viongozi wa juu kwani vitu visiponunuliwa kwa wakati au visipokuwa na ubora hatua zikianza kuchukuliwa zinaanzia kwa viongozi hao hivyo tukiwa na uelewa wa pamoja utasaidia viongozi wetu wasiwajibishwe.

Vile vile Bw. Mbanyi amefafanua kuwa Wakuu wa Idara na Vitengo wana wajibu mkubwa kuhakikisha kwamba taratibu za manunuzi ya umma na thamani ya fedha katika michakato wa manunuzi hayo inapatikana kwani si lengo la Serikali kupata bidhaa na huduma kwa fedha ambazo hazina thamani halisi.

Hata hivyo Bw. Mbanyi ametoa rai kwa waajiri kuhakikisha wanaohusika na manunuzi ya umma katika ofisi zao wawe wamesajiliwa na Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi kwani kutokufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

 Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw.Nicholas William akifungua mafunzo kuhusu Manunuzi ya Umma yanayoendeshwa na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) kwa Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara hiyo kuanzia Mei 27 -28 Jijini Dodoma. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi Tanzania Bw.Godfrey Mbanyi na Kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara hiyo Bw.Orest Mushi.
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) Bw.Godfrey Mbanyi akizungumza na Viongozi wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo wakati Bodi hiyo ilipoendesha mafunzo ya siku mbili kuhusu Manunuzi ya Umma kuanzia Mei 27- 28, 2019 Jijini Dodoma. Katikati ni Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara hiyo Bw.Orest Mushi, na Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ununuzi na Ugavi wa Wizara hiyo Bibi Cecilia Kasonga.
  Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Bw.Orest Mushi akizungumza wakati wa mafunzo ya Ununuzi na Ugavi yanayotolewa na Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (PSPTB) kwa Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara hiyo kuanzia Mei 27- 28 2019 Jijini Dodoma.Katikati ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara hiyo Bw.Nicholas William na Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ununuzi na Ugavi Bw.Godfrey Mbanyi.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw.Nicholas William (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) Bw.Godfrey Mbanyi (wa pili kushoto) na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara hiyo baada ya kufungua mafunzo kuhusu Sheria ya Manunuzi ya Umma yanayoendeshwa na Bodi hiyo kuanzia Mei 27 -28,2019 Jijini Dodoma.