Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu ameingilia kati suala la kukamatwa kwa aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu na kudai suala hilo ni kinyume cha sheria.


Akizungumza kutokea nchini Ubelgiji Tundu Lissu amedai kuwa mikutano ya ndani ambayo Lazaro Nyalandu amekamatwa nayo haijawekewa katazo lolote la kisheria.

"Mikutano ya ndani haijawekewa sharti lolote la kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, kwa taarifa niliyoipata TAKUKURU haijatoa taarifa ni mikutano gani ambayo imekatazwa, na wala hakuna neno linalosema kuwa mikutano iliyokatazwa, badala yake imejipa jukumu Jeshi la Polisi kuilinda," amesema Lissu.

"Tukio la kukamatwa kwa Nyalandu sio la kwanza Singida lakini siku 2 zilizopita viongozi wa Singida Mjini, walikamatwa kwa kutekeleza zoezi wanaloliita "CHADEMA ni Msingi", na Mkuu wa Wilaya Ikungi aliwataka viongozi wa CHADEMA kutoka makao Makuu walioendesha zoezi hilo kuondoka ndani ya Wilaya hiyo na alipoulizwa OCD alieleza kuwa amepewa maagizo", amesema Lissu.

"Kama alivyowahi kusema Jakaya Kikwete na Rais wa awamu iliyopita kuwa CCM ya sasa inategemea nguvu ya polisi kujibu hoja za wapinzani", ameongeza Lissu.

Mapema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU ilitangaza kumshikilia Lazaro Nyalandu, bila kuainisha sababu yeyote ya kukamatwa kwake lakini baadaye walimkabidhisha kwa Jeshi la Polisi.