MASTAA 18 wa kikosi cha Sevilla ya nchini Hispania, jana walitua nchini kwa ajili wa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba.Timu hizo, zinavaana kesho Alhamisi saa moja kamili usiku kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Mchezo huo wa kirafiki umeandaliwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa kwa ushirikiano wa La Liga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).


Akizungumza na Championi Jumatano, Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas alisema maandalizi ya mchezo huo yanakwenda vizuri. Tarimba aliwataja wachezaji waliokuwa kwenye msafara huo kuwa ni Vaclík, Juan Soriano, Sergi Gómez, Kjaer, Gnagnon, Jesús Navas, Aleix Vidal na Escudero.Wengine ni Arana, Amadou, Roque Mesa, Banega, Franco Vázquez, Nolito, Promes, Bryan, Ben Yedder na Munir huku wachezaji watakaosekana ni Wöber, Rog, Carriço na Gonalons na André Silva ambao  ni majeruhi pamoja Sarabia ambaye hayupo fiti tangu atolewe uwanjani dhidi ya Athletic Bilbao.


“Maandalizi ya mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa yanaendelea vizuri na leo (jana) usiku tunatarajiwa kuwapokea wageni wetu Sevilla kutoka Hispania watakapotua nchini.


“Sevilla mara baada ya kutua nchini watafanya utalii mbalimbali kabla na baada ya mchezo huo dhidi ya Simba utakaochezwa keshokutwa (kesho) Alhamisi. “Hivyo, nichukue nafasi hii kuwaomba wadau soka na mashabiki wa Simba kukata tiketi mapema kuepuka usumbufu utakaojitokeza siku hiyo ya mchezo huo,” alisema Tarimba.