Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imewapandisha kizimbani Shamim Mwasha na mume wake, Abdul Nsembo kwa tuhuma za kusafrisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride zenye uzito wa gramu 232.70.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa Serikali, Costantine Kakula mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina, alidai kuwa Mei Mosi mwaka huu kwa pamoja washtakiwa hao wakiwa meneo ya Mbezi Beach walisafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa gramu 232.70 huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Kakula alidai upelelezi bado haujakamilika na aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo Hakimu Mhina alisema washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa kosa wanaloshtakiwa nalo ni la uhujumu uchumi hivyo mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na hawana dhamana.

Wakili wa utetezi, Hajra Mungula aliuomba upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi ili hatua nyingine ziweze kuendelea.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 27, 2019 itakapotajwa tena.