Na  James Ndege - Musoma
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara ameilekeza Mamlaka ya Chakula na Dawa kuanzisha mikakati endelevu ya kuwezesha wajasiriamali wadogo wa mkoa wa Mara  kuzalisha bidhaa zitakazokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi wakati alipofungua mafunzo ya siku mbili yanayoendeshwa na TFDA  kwa wajasiriamali wadogo 100 wa usindikaji wa vyakula wa mkoa wa Mara katika ukumbi wa Mikutano wa Mkoa wa Katibu Tawala wa Mara uliopo mjini Musoma kuanzia tarehe 29 – 30 Mei, 2019.

Maelekezo hayo ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara yalitolewa na mwakilishi wake ambaye ni Kaimu Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa huo, Bw. Denis Nyakisunda aliyekuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyokuwa na lengo la kuwezesha ukuaji wa Sekta ya  viwanda nchini vinavyokidhi vigezo vya usalama na ubora ili kupata soko la bidhaa za Tanzania la  ndani na nje ya nchi hivyo kukuza uchumi wa nchi

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Nyakisunda alisema “Ninafurahi kuona TFDA leo wanatoa mafunzo haya muhimu ili ninyi wasindikaji wa mkoa huu muweze kuanzisha viwanda vidogo lakini pia nawaasa TFDA kuweka mazingira rafiki kwa kuwawezesha wajasiriamali wa mkoa wangu kutatua changamoto walizonazo katika uanzishaji wa viwanda vidogo vya vyakula”.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula kutoka TFDA Makao Makuu, Bw, Lazaro Mwambole aliwapongeza wasindikaji hao kwa kujitokeza kwa wingi katika mafunzo hayo na kuwaasa kuzingatia ushauri wa wataalam katika kuzalisha bidhaa zao ili ziweze kusajiliwa na TFDA hivyo kupata soko la ndani na nje ya nchi.

 “Mkizingatia mada za mafunzo zinazotolewa hapa na kushirikiana kwa pamoja, suluhisho la changamoto hizo zitabadilika kuwa fursa. Ofisi ya TFDA Kanda ya Ziwa Mashariki pamoja waratibu wa majukumu ya TFDA katika Halmashauri zenu wapo nanyi siku zote hivyo watumieni kupata huduma na ushauri mara kwa mara” alihitimisha kiongozi huyo.

Mafunzo husika yamefungwa na Meneja wa SIDO wa mkoa wa Mara Bi. Frida Mungulu ambaye alipokea maazimio sita kutoka kwa washiriki ili yafanyiwe kazi katika ngazi mkoa kwa nia ya kupata ufumbuzi wa changamoto za uanzishaji viwanda kwa wajasiriamali hao.
Katika mafunzo hayo, TFDA ilishirikisha Taasisi nyingine za Serikali za Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Tantrade ili kuwawezesha wasindikaji hao kutambua mambo muhimu yanayotakiwa katika kuzalisha bidhaa zinazokubalika kwa mujibu wa sheria zilizopo. Mafunzo hayo ya TFDA ni endelevu na mkoa wa Mara umekuwa mkoa wa 26 nchini kupata mafunzo ya aina hiyo.
 Mgeni Rasmi katika Mafunzo hayo, Mwakilishi wa  Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Denis Nyakisinda akisisitiza jambo kwa wajasiriamali (hawapo pichani) katika hotuba ya ufunguzi wakati mafunzo ya siku mbili yanayoendeshwa na TFDA  kwa wajasiriamali wadogo 100 wa usindikaji wa vyakula wa mkoa wa Mara katika ukumbi wa Mikutano wa Mkoa wa Katibu Tawala wa Mara
 Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula TFDA, Bw. Lazaro Mwambole akiwasilisha mojawapo ya mada kwa washiriki wakati wa mafunzo ya siku mbili yanayoendeshwa na TFDA  kwa wajasiriamali wadogo 100 wa usindikaji wa vyakula wa mkoa wa Mara katika ukumbi wa Mikutano wa Mkoa wa Katibu Tawala wa Mara. 
Sehemu ya washiriki wakifuatilia mada katika mafunzo ya siku mbili yanayoendeshwa na TFDA  kwa wajasiriamali wadogo 100 wa usindikaji wa vyakula wa mkoa wa Mara katika ukumbi wa Mikutano wa Mkoa wa Katibu Tawala wa Mara.
 Picha ya pamoja baina ya wajasiriamali na wawakilishi wa taasisi za Serikali katika mafunzo hayo. Waliokaa ni Mgeni Rasmi  aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara,  Denis Nyakisinda (Katikati), Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula TFDA, Bw. Lazaro Mwambole (wa kwanza kushoto) na Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Bi. Nuru Mwasulama.