KOCHA Mkuu wa timu ya Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema kuwa hamna namna yoyote ambayo Simba wataweza kuwazuia wasiwafunge kwani mbinu zao wanazijua hivyo ni lazima wakae.

Kagera Sugar itamenyana na Simba leo Uwanja wa Uhuru wakiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 uwanja wa Kaitaba.

Akizungumza na Saleh Jembe, Maxime amesema kuwa hawana hofu na kikosi cha Simba kwani wanatambua mbinu zao hivyo hawatapata taabu kupata matokeo.

"Naitambua vizuri Simba, najua mbinu zao na sehemu ya kuwabana ili kuwafunga tena mabao mengi ili kujiweka sehemu nzuri kwenye ligi, kama ambavyo niliwasumbua nyumbani nitafanya tena ugenini ili kuweka heshima kwa kikosi changu.

"Mwanzo wetu ulikuwa mbovu wakatubeza nadhani sasa watashtuka kidogo ila bado kazi ipo palepale nimewaambia wachezaji wangu, mchezo ni wetu na tunataka matokeo hakuna kinachoshindikana, mashabiki wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti," amesema Maxime.

Kagera Sugar ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi kuu baada ya kucheza michezo 34 imejikusanyia pointi 43, imeweka rekodi ya aina yake kwa kuifunga Simba mabao zaidi ya mawili msimu huu kwenye mechi 31 ambazo Simba imecheza.