Uongozi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara umelazimika kufunga kamera maalumu katika maeneo yote ya hospitali hiyo ili kukabiliana na matatizo ya wizi wa vifaa tiba na dawa pamoja na vipigo kutoka kwa ndugu wa wagonjwa dhidi ya baadhi ya wauguzi pindi wanapobainika kutoa huduma za matibabu zisizoridhisha.

Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dk. Joakim Eyembe akizungumza na wauguzi baada ya kusikiliza kero zinazowakabili kuhusiana na vitisho toka kwa ndugu wa wagonjwa na wizi wa vifaa tiba na dawa, amewaondoa hofu kwa kuwaambia tayari kamera zimefungwa kila sehemu.

Dk. Eyembe akizungumza kupitia kilele cha maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani katika viwanja vya hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara, ameongeza kuwa wameamua kuajiri kampuni maalumu ya ulinzi ili kuweza kukabiliana na tatizo la wizi wa vifaa tiba unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watu wanaoingia kwa kupitia katika uzio.

Wauguzi katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara iliyopo mjini Musoma wamekuwa wakitoa huduma za afya kwa wagonjwa wengi kwa wakati mmoja kutokana na kuwa wachache wao baada ya zoezi la serikali kukabiliana na tatizo la vyeti feki.