Waziri wa habari, sanaa, vijana, utamaduni na michezo Dkt.Harrison Mwakyembe akizungumza katika jukwaa la tafakuri katika maadhimisho ya siku ya Afrika duniani ambapo amewataka vijana kujituma na kuwa wazalendo katika kuhakikisha rasilimali zinalindwa na kutumika ipasavyo, leo jijini Dar es Salaam.
 Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda akitoa majumuisho ya mdahalo huo ambapo ameeleza kuwa hakuna budi kudhibiti rasilimali za asili kwa umakini na kuweka sera elekezi za biashara katika rasilimali hizo, leo jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Misri Nchini Tanzania Gaber Mohamed akitoa neno katika mjadala huo, amehimiza umoja na mshikamano miongoni mwa nchi za Afrika, leo jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi mtendaji mkuu wa makampuni ya Uhuru Media ambao pia ni waandaaji wa jukwaa hilo Ernest Sungura akizungumza wakati wa jukwaa hilo na kusema kuwa wanategemea matokeo chanya na ya kujenga kupitia mdahalo huo, leo jijini Dar es Salaam.
 Balozi mstaafu Christopher Liundi akichangia mada katika jukwaa hilo, Balozi Liundi amesema kuwa malezi bora yanajenga uzalendo na kuwataka vijana  kujituma katika kazi, leo jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa magazeti ya serikali Zanzibar Mahfoudha Hamid akichangia mada katika mjadala huo, leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti mstaafu wa bunge la Afrika Mashariki Getrude Mongella akichangia mada katika jukwaa hilo ambapo amewataka vijana kuwa wazalendo na kubeba taifa kuelekea mafanikio, leo jijini Dar es Salaam.



 Baadhi ya mabalozi pamoja na wageni waalikwa wakifuatilia mada

MAADHIMISHO ya siku ya Afrika yanayoadhimishwa kila tarehe 25 mwezi Mei, kwa mwaka huu yameadhimishwa kwa jukwaa la tafakuri lenye kauli mbiu ya "Uafrika wetu na rasilimali za Bara letu ni urithi wetu" huku vijana wakipata somo kutoka kwa wazee na wapigania uhuru wa taifa.

Akizungumza katika tafakuri  hiyo ya pili Waziri wa Habari, sanaa, vijana utamaduni na michezo Dkt. Harison Mwakyembe amesema kuwa viongozi wa Afrika watakumbukwa kwa mengi waliyoyafanya pamoja na juhudi na jitihada walizozifanya zitaishi daima na kumbukumbu zao zitahifadhiwa daima na hadi sasa  zaidi ya kumbukumbu 256 zimehifadhiwa na amewataka vijana kujifunza kutoka kwa watetezi hao.

Mwakyembe amesema kuwa wao kama wizara wataendelea kuhifadhi mazuri yote yaliyofanywa pamoja na kuyaendeleza na hiyo ni pamoja na kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa Lugha inayounganisha bara la Afrika.

Aidha amesema kuwa vijana lazima wawe nguzo imara na wazalendo katika kuhakikisha rasilimali zinanufaisha jamii za kiafrika.

Akizungumza katika halfa hiyo Mkurugenzi mtendaji mkuu wa makampuni ya Uhuru ambao ni waandaaji wa jukwaa hilo Ernest Sungura amesema kuwa imepita miaka 56 tangu nchi za Afrika kujikomboa na ni muhimu sana kwa vijana kurithi mawazo na fikra pana kutoka kwa wazee na watetezi wa taifa.

Amesema kuwa baada ya kujikwamua kisiasa sasa ni wakati wa kujikwamua kiuchumi ambapo Rais wa awamu ya tano Rais Dkt.John Magufuli anaonesha nguvu na nia ya kujikomboa kiuchumi, amesema kuwa Rais Magufuli atakumbukwa na kushukuriwa daima kwa uthubutu na ujasiri wake katika kupambana na masuala yanayokwamisha kukua kwa uchumi ikiwemo kupinga ufisadi, rushwa na ulevi wa madaraka.

Sungura amesema kuwa  kupitia jukwaa hilo matokeo yanayotarajiwa na pamoja na kuona uhifadhi wa historia, tamaduni na rasilimali, ukombozi wa kisiasa na kiuchumi katika zama hizi mpya pamoja na kulinda haki na usawa hasa kwa wanyonge.

Kwa upande mwenyekiti mstaafu wa Bunge la Afrika Mashariki, Getrude Mongella amesema kuwa jambo linalofanya Afrika kubaki tegemezi hasa kwa wanawake ni kwamba; wanaume waliopewa jukumu la kuongoza Afrika walituangusha hivyo vijana wa sasa wawe shupavu ili kuwatoa wanaafrika kutoka sehemu moja kwenda yenye matumaini zaidi.

Getrude amesema kuwa huu ni wakati wa kazi tuu na sio  wakati wa kuoneshana vidole bali wakae na kufikiri ni wapi pamekwama pamoja na kujitambua na kujituma katika kutumia rasilimali katika kujikwamua kiuchumi.

 Mwenyekiti wa kigoda cha Mwalimu Nyerere Profesa. Rwekaza Mukandala amesema kuwa historia ya siku hiyo ya Afrika  ni muhimu kwa vijana katika kurithi yaliyo mema kutoka kwa wazee na hasa uzalendo na ushujaa katika kuleta maendeleo.

Mukandala amesema kuwa mwaka 1963 tarehe kama ya leo takribani nchi 32 zilikuwa huru na ndipo umoja wa nchi huru za Afrika(OAU) ulianzishwa.

Mukandala amesema kuwa mapambano ya kisiasa yalipita na kwa sasa hatuna budi kutumia rasilimali zetu ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kujitegemea kupitia uchumi wetu.

Kwa upande wake balozi mstaafu Christopher Liundi amesema kuwa uzalendo hasa kwa vijana ni lazima kuzingatia elimu za aina tatu zikiwemo elimu kutoka nyumbani, elimu ya darasani na elimu dunia, amesema kuwa malezi bora huanzia nyumbani na ndio huzaa uzalendo.

Amesema kuwa vijana lazima wasome ili waweze kutofautisha mazuri na mabaya pamoja na kulitumikia taifa kwa moyo wote.

Aidha imeelezwa kuwa kitu kinachokwamisha muunganiko huo wa Afrika ni pamoja na ulafi wa madaraka na ubinafsi huku Tanzania ikitolewa mfano kwa kuwa nchi inayofuata misingi ya demokrasia na uongozi.