KIJANA Hamisi Ligwila (18), mkazi wa Yombo Makangarawe anayesumbuliwa na tatizo la miguu kuvimba, amerudishwa nyumbani baada ya kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, zaidi ya mwezi mmoja ambapo amewaomba Watanzania wazidi kumuombea.Akizungumza na Nivushe, Hamisi alisema kuwa anamshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kuweza kumsaidia mpaka kufika hospitalini hapo  na kuchukuliwa vipimo mbalimbali.“Namshukuru sana mheshimiwa Makonda, aliacha muda wake na kuwaambia watu wake kunisimamia mpaka kufika Hospitali ya Muhimbili lakini sasa nimerudi nyumbani,” alisema Hamisi.Akiendelea kuzungumza na Nivushe, Hamisi ambaye kwa sasa anaishi na dada na kaka yake ambao wanamuangalia, alisema kuwa ameruhusiwa kurudi nyumbani lakini bado anahitaji sana msaada wa karibu kutoka kwa Watanzania wenzake kwani anakabiliwa na changamoto nyingi sana za kibinadamu.“Nimer-uhusiwa kutoka hospitali lakini bado nina changamoto nyingi hapa ninapoishi, natakiwa kodi na hata chakula cha kila siku maana hapa nilipo sijajua hatima yangu kwa sababu kule Muhimbili hawakunipa majibu yangu,” alisema Hamisi.Hamisi aliongeza kuwa ndugu zake wanaomsaidia wanashindwa kwenda kutafuta riziki kwa sababu wanamuangalia na mama yake mzazi aliyekuwa akimuangalia kwa ukaribu, naye anaumwa na amepelekwa nyumbani kwao Mtwara.Awali, Hamisi aliwahi kwenda India kufanyiwa upasuaji wa kupunguzwa uvimbe miguuni nchini kisha kurudishwa nchini lakini baadaye hali ilibadilika na miguu yake kuvimba tena.

Kama umeguswa na tatizo linalomsumbua Hamisi kwa muda mrefu unaweza kumsaidia chochote kupitia namba yake ya mkononi 0672960399.