Uhasama wa Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya makampuni makubwa ya mawasiliano kutoka China umeanza kuiweka kampuni ya simu za mkononi ya Huawei katika matatizo makubwa.

Kampuni ya Kimarekani ya Google imetangaza kuizuia Huawei kutumia toleo jipya la programu ya kuendesha simu za mkononi ya Android, hiyo ikiwa na maana kuwa kampuni hiyo ya Kichina haitapata tena ruhusa ya kutumia programu hiyo muhimu katika simu zake mpya.

Marekani inashuku kuwa Huawei huweka katika vifaa inavyovitengeneza, programu za siri za kijasusi zinazoweza kuhatarisha usalama wake wa taifa.

Huawei inazikanusha shutuma hizo. Katika tangazo lake la hivi punde, Huawei imesema itaendelea kutoa huduma za kiusalama kwa watumiaji wa simu zake ambazo tayari zimekwishanunuliwa, na zile ambazo bado ziko madukani.