Idara ya Masoko nchini Marekani imetangaza kutoa leseni ya siku 90 kwa makampuni ya simu na watoa huduma za mtandao kufanya kazi na kampuni ya Huawei ili kuendelea kuziweka data zake hewani na kulinda usalama wa watumiaji.

Kutokana na leseni hiyo, sasa Google inaruhusiwa kutuma mabadiliko yake mapya ya kimfumo kwa simu za Huawei, ikiwa ni pamoja na mfumo wa 'Android Operating System' hadi Agosti 19.

Msemaji wa Google ameuambia mtandao wa CNBC mapema leo Jumanne kuwa, "kuendelea kubadilisha mifumo ya simu na usalama ni wazo la kila mmoja wetu na kwa hii leseni ya muda mfupi inaturuhusu kuendelea kutoa huduma za kimtandao na mifumo ya ulinzi kwa siku 90 zijazo".

Pia Idara Masoko nchini Marekani imesema kuwa itafikiria kuongeza au kutoongeza leseni hiyo baada ya siku 90 zilizotolewa kuisha.

Takwimu zinaonesha kuwa kati ya $70 bilioni ambazo kampuni ya Huawei imetumia kununua vifaa vya simu mwaka 2018, $11 bilioni zilikwenda kwa makampuni ya Marekani ikiwemo Qualcomm, Intel na Micron. Kwa mujibu wa takwimu za Canalys, zaidi ya asilimia 49 ya simu za Huawei zimesafirishwa nje ya nchi ya China katika kipindi cha robo ya mwaka 2019.

Huawei, ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya binafsi China imekuwa ikihusishwa na kutumika na serikali ya China. Marekani na baadhi ya washirika wake wamekuwa wakidai kuwa teknolojia ya Huawei inatumika na mashirika ya ulinzi ya China kwa upelelezi.

Hata hivyo mwanzilishi wa kampuni ya simu ya Huawei, Ren Zhengfei amekanusha vikali tuhuma hizo akisema kuwa kukubali kufanya upelelezi ni hatari ambayo asingeweza kuifanya.