Arsenal na Chelsea tayari wako jijini Baku kwa ajili ya fainali ya Europa usiku wa leo, London ni jiji la pili tu kuwahi kufikisha timu mbili katika fainali ya mashindano ya vilabu Ulaya.
Madrid ndio lilikuwa jiji la kwanza na wamefanya hivyo mara mbili, 2014 na 2016 ambapo Real na Atletico walifika fainali pamoja, lakini mwaka huu ni zamu ya London.

Kocha wa Arsenal Unai Emery, ambaye amewahi kushinda Kombe hilo mara tatu mfululizo akiwa na Sevilla ana changamoto kubwa kwenye kupanga kikosi chake katika nafasi ya mlinda mlango. Pert Cech, ambaye amekuwa akidaka kwenye mechi za Europa, anahusishwa kujiunga na Chelsea kwenye nafasi ya Mkurugenzi wa Ufundi.

Baadhi ya wachambuzi wanashauri Emery kutokana na hali ilivyo amuanzishe mlinda mlango chaguo la kwanza Bernd Leno nafasi ya kuanza kwenye mchezo huo jijini Baku.
Emery atamkosa kiungo mshambuliaji Henrikh Mkhitaryan, ambaye hakusafiri na timu inayokwenda kucheza katika dimba la Olympic Stadium kwenye mji mkuu wa Azerbaijan.

Mkhitaryan ambaye ni raia wa Armenia – nchi ambayo haina mahusiano mazuri ya kidiplomasia na Azerbaijan. Nchi hizo pia zina ugomvi ambao unaendelea hadi sasa wakigombania ukanda ambao upo ndani ya mipaka ya Azerbaijan.

Naye kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri atawakosa baadhi ya wachezaji wake. Chelsea ambao walicheza mechi ya hisani nchini Marekani baada ya msimu wa ligi kuisha na kiungo Ruben Loftus-Cheek kuuma huku wakishinda kwa magoli 3-0 dhidi ya New England Revolution.
Wengine watakaokosekana kwenye kikosi cha Chelsea ni beki Antonio Rudiger na Callum Hudson-Odoi, huku Ng’olo Kante akiwa bado hajaanza mazoezi magumu.

“Mara nyingi mchezo dhidi ya Arsenal huwa uko wazi. Wana washambuliaji wazuri sana, Aubameyang pamoja na Lacazette. Timu yao inashambulia vizuri sana na pia wana uwezo wa kukaba kuanzia kwa timu pinzani, kwa hiyo sio rahisi kucheza dhidi yao. Kocha wao amefanya kazi nzuri sana, hivyo ni mchezo mgumu.” Maurizo Sarri.

Chelsea wao wameshafuzu kucheza katika Kombe la Mabingwa Ulaya, Arsenal hii ndiyo nafasi yao ya mwisho kupata tiketi ya kushiriki UEFA Champion League. Hata hivyo Sarri huenda ikawa nafasi yake ya mwisho kutetea kibarua chake pia. Bonge la Mechi.
Mchezo utapigwa leo Jumatano saa 4:00 Usiku katika dimba la Olympic Stadium jijini Baku. Na utarushwa moja kwa moja kupitia StarTimes World Football katika kingamuzi cha StarTimes pekee.

Kwa wateja wa dikoda za Antenna watatakiwa kulipia kifurushi cha UHURU kwa Tsh 18,000 tu na kwa wateja wa dish watalipia kifurushi cha SMART kwa Tsh 21,000 pekee.