MSANII wa Bongo Fleva, Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ amefichua siri yake na msanii mwenzake, Faustina Charles ‘Nandy’ kwa kusema kuwa akiwa naye popote pale familia yake huwa na amani.Dogo Janja aliyazungumza hayo leo katika mahojiano na kipindi cha Bongo 255 kinachoruka kupitia +255 GLOBAL RADIO ambapo alisema kuwa, alijuana na Nandy kabla hata hajaanza muziki.


“Nandy ni mshikaji wangu tangu zamani sana. Nakumbuka tangu hajaanza muziki wala kushiriki yale mashindano ya kuimba ambayo yalimtoa (Tekno Own Stage) yaliowahi kufanyika nchini Kenya na Nigeria.“Ujue damu zetu zinaendana sana na ni mtu ambaye hata familia zetu zinafahamiana. Leo Nandy atakuja kwetu na mimi hivyohivyo kwao kwa hiyo hata nikiwa naye popote familia yake inakuwa na amani kabisa,” alisema Dogo Janja.


Mbali na hilo, Dogo Janja pia alimuongelea msanii wa Bongo Fleva, William Lyimo ‘Billnass’ ambaye alidaiwa kutoka na Nandy kipindi cha nyuma kuwa akimuonea wivu atashangaa sana.


“Billnas hata akihisi kitu chochote kibaya kwangu mimi na Nandy atakuwa ni mtu wa ajabu sana. Ngoja nikwambie kitu, nikiwa na Nandy hakuna chochote kibaya kinaweza kutokea kati yetu,” aliongeza Dogo Janja