WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Mawasiliano Barani Afrika Jijini Dar es Salaam.
Watu waliohudhuria katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Mawasiliano Barani Afrika Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Chama cha Maafisa Uhusiano wa Sekta binafsi Tanzania (PRST) Loth Makuza katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Mawasiliano Barani Afrika Jijini Dar es Salaam. 
Leah Mushi akizungumza machache.
Mwenyekiti wa TAMWA na Mhariri Mkuu wa Clouds Fm Joyce Shebe akizungumza machache.
Picha ya viongozi na Dkt. Mwakyembe.
Picha ya pamoja na washiriki.

 WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na wanahabari.

Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka maofisa habari kupitia vyombo vya habari kuendelea kutangaza maendeleo na mafanikio ya nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania.

Akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Mawasiliano Barani Afrika Jijini Dar es Salaam, Dkt. Mwakyembe amesema vyombo vya Habari vya Afrika havina budi kuonyesha udhubuti kwa kuweka sera zinazoakisi maendeleo na kuyatangaza kwa Wananchi wake na wote waliopo nje ya Bara hilo.

Dkt. Mwakyembe amesema sehemu kubwa ya maudhui ya Vyombo vya Habari vilivyopo nje ya Bara la Afrika vinavyoongozwa na Wakoloni waliowahi kutawala katika Bara la Afrika hawapendi kuona Nchi za Afrika zinapiga hatua za Maendeleo kwa wananchi wake na badala yake hupenda kuripoti na kutangaza mambo mabaya yanayohusu Afrika ikiwemo njaa, magonjwa, vurugu za kisiasa, vita n.k.

Aidha Dkt. Mwakyembe amesema yapo mambo mazuri ya Maendeleo yanayofanyika katika Nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania ambayo zimepiga katika kipindi cha miaka minne imepiga hatua kubwa katika Maendeleo ya kiuchumi, na miundombinu, jambo ambalo baadhi ya vyombo vya habari vya Mataifa ya Nje ya Afrika yamekuwa hayapendi kuyatangaza, hivyo ni wajibu wa vyombo vya habari kutumia majukwaa yao kutetea na kutangaza mafanikio hayo.

“Wakati Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Kenneth Kaunda wa Zambia walipoamua kujenga Reli ya Tazara, walipingwa vikali sana Wakoloni waliotuwala na wengine waliita reli ile kuwa ni bamboo (mianzi) lakini ni taifa moja tu la Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China walitusaidia na leo hii reli ile ndiyo ndefu zaidi katika Bara la Afrika yenye urefu wa kilometa 1860” alisema Dkt. Mwakyembe.

Kwa mujibu wa Waziri Mwakyembe alisema Maendeleo ya Bara la Afrika yatatetewa na kupiganiwa na Wafrika wenyewe, hivyo ni wajibu wa vyombo vya habari vya Bara hilo kujitokeza na kutetea Maendeleo hayo na kamwe haitatokea siku moja chombo cha habari cha BBC au CNN vikatangaza mafanikio hayo kwani hawapendi kuona Mataifa waliyoyatawala yakifikia hatua kubwa za kimaendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, alisema Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za mawasiliano katika sekta binafsi ili kuhakikisha kuwa wanajenga daraja moja katika kusukuma mbele gurudumu la Maendeleo ya sekta ya habari na Mawasiliano nchini.

Naye Rais wa Chama cha Maafisa Uhusiano wa Sekta binafsi Tanzania (PRST) Loth Makuza alisema, taasisi hiyo ni jukwaa huru linalotoa fursa na nafasi ya kujadili masuala mbalimbali ya mawasiliano nchini ikiwemo changamoto na utatuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya habari na mawasiliano nchini.

Anaongeza kuwa Taasisi hiyo kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano imeweza kutengeneza majukwaa mbalimbali yanayotangaza masuala mbalimbali ya kimaendeleo yaliyofikiwa katika Nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania, lengo likiwa ni kubadili mtazamo hasi wa Bara la Afrika katika nyanja za kiuchumi, kijamii kupitia ngazi ya kimataifa na duniani kwa ujumla.