Mahakama nchini Kenya imemuamuru rais wa zamani wa Kenya kulipa fidia ya dola milioni 1.06 kwa mjane ambaye alimchukulia ardhi yake kenyume cha sheria

Bwana Moi alinyakua ardhi ya heka 53 iliyokuwa mali ya mjane Susan Cheburet Chelugui, alisema Jaji.

Bwana moi alinyakua ardhi hiyo kinyume cha sheria miaka 36 iliyopita, lakini ilisajiliwa kwa jina la Bana Moi mwaka 2007.

Rais huyo wa zamani ambaye ndiye rais aliyekuwa mamlakani kwa muda mrefu zaidi , alishutumiwa na Bi Chelugui na mtoto wake wa kiume David Chelugui kwa kusajili ardhi ya familia yao kwa jina lake miaka miwili baada ya Bwana yake Bi Chelugui kufariki dunia.

Inasemekana baadae Bwana Moi aliiuza ardhi hiyo kwa kampuni ya utengenezaji wa mbao Plywood Limited.

Kampuni ya Rai Plywood Limited iliwaeleza majaji kuwa ilinunua ardhi hiyo kutoka kwa Moi mnamo mwaka 2007 baada ya kufanya uchunguzi wa kina wa kisheria kuhusu ardhi hiyo.

Hata hivyo, Bwana Moi hakuweza kuipatia mahakama ushahidi wowote juu ya jinsi alivyopata ardhi, anasema mwandishi wa BBC Mercy Juma aliyepo Nairobi.

Jaji Anthony Ombwayo alisema Bwana Moi alikuwa na mienendo ya "isiyo ya kawaida, ukiukaji katiba, kutofuata utaratibu " na "yenye dosari ".

Bwana Moi alikuwa rais wa pili wa Kenya mwaka 1978 ambapo alihudumu hadi mwaka 2002.