MAMBO vipi mpenzi msomaji wangu, kama ujuavyo, kawaida ya safu hii ni kukuwekea wazi maisha halisi wanayoishi mastaa mbalimbali wa hapa Bongo na watoto wao.  Leo tunaye muigizaji wa muda mrefu, Chuchu Hans ambaye tayari amebarikiwa watoto watatu huku mmoja akiwa amezaa na muigizaji maarufu Bongo, Vincent Kigosi ‘Ray’. Msanii huyo amezungumza mambo mengi sana kuhusiana na maisha yake na watoto wake huku akionyesha wazi kuwa ni mama bora. Fuatilia mahojiano hapa chini;

Wikienda: Wewe ni mama wa watoto watatu lakini baba ni tofauti, unawezaje kuwalea? Je, wanaelewa nini katika hilo?

Chuchu: Uzuri ni kwamba watoto wangu hawana ubaguzi wa kusema huyu baba yake ni yule na huyu baba yake yule, wote wanajiona kama ni wa mama na baba mmoja kwa sababu hata baba yao ambaye yuko karibu anawaangalia wote kwa pamoja tu.

Wikienda: Siyo kwamba baba wa mtoto mmoja anafanya vitu vingi kwa mtoto wake kuliko wengine?

Chuchu: Yaani katika hilo namshukuru sana Mungu ameniepushia, kwa sababu hata ukimkuta yule mtoto wangu wa pili na baba Jaden utasema ni wake kabisa na anajua hivyo na nimewatengenezea waishi hivyo kwa sababu hata wakija kuwa wakubwa wasiwe na tofauti

watoto wako wote watatu ni mmoja tu, tena yule wa kwanza ndio anafanana na wewe lakini wengine ni baba zao, hii imekaaje?

Chuchu: Mimi naona sawa, tena kama Jaden alivyofanana na baba yake napenda sana na hiyo inampa baba imani kubwa kuwa hajaibiwa.

Wikienda: Unawalea watoto wako katika maadili gani? Ya kistaa au maisha ya kawaida?

Chuchu: Kwanza kabisa mimi mwenyewe kuna wakati najisahau kabisa kama ni staa hivyo na watoto wameichukulia hivyo na maisha yao ni ya kawaida sana na nimependa kuwalea hivyo maana kuna leo na kesho.

Wikienda: Nini unataka watoto wako wajifunze katika maisha yao hata ukiwa haupo?

Chuchu: Kikubwa wajifunze upendo kuwa ndio kila kitu na kingine wawe na busara maana hubeba kila kitu katika maisha.

Wikienda: Una mpango wa kuongeza mtoto mwingine?

Chuchu: Hapana, Jaden ndio wa mwisho, sasa hivi nataka kufanya kazi zaidi na si kitu kingine.

Wikienda: Unapenda watoto wako wote wafuate nyayo zako?

Chuchu: Hapana! Nataka kila mmoja achague anachotaka, kama wa kwanza alivyopenda kuigiza nilimuacha kwa sababu ni kitu ambacho alikipenda mwenyewe.

Wikienda: Ni mikakati gani unafanya kwa ajili ya watoto wako?

Chuchu: Hakuna kitu ninachokipenda kama elimu nzuri kwa watoto wangu, hivyo nafanya vitu vingi ili tu watoto wangu wasome vizuri.

Wikienda : Asante sana Chuchu kwa ushirikiano wako.

Chuchu: Asante sana na karibu