Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Pato la Taifa kwa Mwaka 2019 linatarajiwa kukua kwa kasi ya wastani wa asilimia 7.8% itakayosababisha kuimarika zaidi kwa Uchumi wa Zanzibar kutokana na ongezeko la Uwekezaji katika Sekta ndogo ya usafirishaji na Uvuvi.

Alisema hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa Pato la Mwananchi mmoja mmoja kutoka Shilingi Milioni 2,104,000/- sawa na Dola za Kimarekani Mia 944 na kufikia Shilingi za Kitanzania Milioni 2,323,000/- sawa na Dola za Kimarekani Elfu 1.026.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika Kibao cha Bajeti 2019/2020 kilichoanza Baraza la Wawakilishi Chukwani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar tayari imekaribia kufikia kiwango cha Nchi ya kipato ca Kati cha Dola za Kimarekani Elfu 1,030 kwa mujibu wa vigezo vya Kimataifa.

Balozi Seif alisema Pato la Taifa kwa bei ya soko limefikia thamani ya Shilingi Bilioni 3,663,000,000/- kwa Mwaka 2018 kutoka thamani ya Shilingi Bilioni 3,228,000,000/- kwa Mwaka 2017 kulikosababishwa na ongezeko la pato la Mwananchi.

Alisema kasi ya mfumko wa bei pia umeshuka hadi kufikia wastani wa asilimia 3.9 Mwaka 2018 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.6 Mwaka 2017 baada ya kuchukuliwa hatua za udhitibi wa mfumko wa bei kwa kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula.

Balozi Seif alisema hali hiyo inatokana na uwezeshwaji waliopatiwa Wakulima kwa kupatiwa pembejeo na mafunzo ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia Teknolojia ya gharama nafuu iliyokwenda sambamba na utafiti katika Sekta ya Kilimo uliosaidia kupata mbinu za kupiga vita changamoto zinazoyakabili mazao ya matunda na mboga za majani.

Alieleza kwamba Muelekeo wa Hali ya Uchumi wa Zanzibar kwa Mwaka 2019 unategemewa kwenda sambamba na Utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2020, Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanzibar {MKUZA 111} na ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduai ya Mwaka 2015 – 2020.

Balozi Seif alifahamisha kuwa mafanikio yote yaliyopatikana yanatokana na jitihada kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Uongozi mahiri wa Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein katika kuona hali ya uchumi na Kijamii ya Taifa na Wananchi inazidi kuimarika kila kukicha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba azma ya Serikali kuu ni kuhakikisha kwamba inakamilisha Miradi yote mikubwa ya Maendeleo kama ilivyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020.

Aliitaja Miradi hiyo kuwa ni pamoja na Ujenzi wa Jengo la Abiria {Terminal 3} katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Zanzibar, Ujenzi wa Bandari ya Mpiga Duri iliyopo Maruhubi pamoja na Ujenzi wa Hospitali Binguni iliyopo Wilaya ya Kati.

Alisema miradi hiyo inakwenda sambamba na mpango wa Taifa wa kuendelea kuimarisha uzalishaji na usafirishaji wa zao la Karafuu kutokana na matarajio ya msimu mkubwa wa zao hilo kwa Mwaka huu wa 2019 pamoja na kupanuka kwa kiwango cha idadi ya Watalii kutokana na kupatikana kwa masoko mapya ya sekta hiyo.

Balozi Seif alifafanua wazi kwamba Serikali tayari imeandaa mikakati maalum ya kutafuta fedha kwa Nchi na Mashirika rafiki sambamba na kutenga Fedha kutoka katika vianzio vyake vya ndani ili itapotokezea kushindikana kupata msaada kutoka nje Serikali iendelee na ukamilishaji wa Ujenzi wa Miradi hiyo.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa Mchanga, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema mchanga ni Rasilmali muhimu hapa Nchini kutokana na matumizi makubwa katika Sekta ya Ujenzi.

Balozi Seif alisema kwa bahati mbaya eneo halisi linaloweza kuchimbwa mchanga katika Visiwa vya Zanzibar ni dogo zaidi kwa kuwa baadhi ya maeneo mengine tayari yameshachimbwa, wakati mwengine yanatumika kwa matumizi ya Kibinaadamu ikiwemo Makaazi, Kilimo na Huduma za Kijamii.

Alisema kutokana na changamoto hiyo Serikali Kuu ililazimika kutangaza utaratibu Mpya wa usimamizi wa uchimbaji, usafirishaji na uuzaji Mchanga ulioanza Tarehe 3 Machi Mwaka 2017 kwa lengo la kujaribu kudhibiti maeneo ya Ardhi na kuweza kutumika kwa shughuli nyengine hasa Kilimo.

Alifahamisha kwamba tokea kuanza kwa utaratibu huo unaosimamiwa na Serikali Kuu yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana ikiwemo gari zinazobeba mchanga kupimwa ili kupata Takwimu na malipo sahihi ya bidhaa hiyo, kupunguza msongamano wa Gari machimboni pamoja na uwepo wa bei elekezi inayowazuia Wafanyabiashara kupandisha bei ya mchanga kiholela ambayo huwaumiza Wananchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliweka wazi kwamba katika kipindi cha kuanzia Mwezi Machi 2017 hadi Disemba 2018 chini ya usimamizi huo jumla ya Tani Milioni 1,690,122 za Mchanga zilichimbwa Visiwani Zanzibar.

Alisema kati ya Tani hizo Unguja ilichimbwa na kusafirishwa Tani Milioni 1,605,517 na Pemba zilizchimbwa na kusafirishwa Tani 84,605 sawa na asilimia 5% ya uchimbaji unaofanyika katika Kisiwa cha Unguja.

“ Kwa Takwimu hizi ni wazi kwamba ipo kasi kubwa ya uchimbaji wa mchanga katika Kisiwa cha Unguja ikilinganishwa na uchimbaji wa Mchanga katika Kisiwa cha Pemba”. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Wananchi kwamba Serikali haitamvumilia Mtu ye yote yule ambae atachimba na kusafirisha mchanga kinyume na utaratibu uliowekwa au kuuza mchanga kinyume na bei elekezi iliyowekwa na Serikali.

Kuhusu Sekta ya Elimu Balozi Seif alisema Serikali Kuu kupitia Wizara inayosimamia Taaluma inaendelea kuchukuwa hatua kadhaa katika kuhakikisha mazingira ya Elimu yanakuwa mazuri ili Watoto wa Visiwa vya Zanzibar waweze kupata Haki yao ya Elimu bila ya Malipo.

Alisema inapendeza kuona asilimia ya Uandikishaji katika ngazi zote za Elimu ya lazima imeongezeka ikilinganishwa na Mwaka wa Fedha wa 2017/2018 ambapo ngazi ya Maandalizi uandikishaji umefikia asilimia 69.4% Mwaka 2018 kutoka asilimia 66.1 Mwaka 2017.

Balozi Seif alieleza kwamba kasi hii ya uandikishaji inatokana na upatikanaji wa nafasi, mwamko wa Jamii kuhusu Elimu na ushiriki mzuri wa Wananchi katika kuleta Maendeleo kwenye Sekta ya Elimu.

Alieleza kwamba katika juhudi za kuimarisha Sekta hiyo muhimu kwa Taifa lolote lile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Mfuko wa OPEC tayari imekamilisha ujenzi wa Skuli Tisa za Ghorofa za Sekondari Unguja na Pemba.

Alisema Mradi huo mkubwa umekwenda sambamba na ujenzi wa Maabara, Maktaba na vyumba vya Kompyuta kwa Skuli 24 za Sekondari kwa mashirikiano na Benki ya Dunia.

Balozi Seif alifahamisha kwamba katika kuimarisha Elimu ya Sekondari Serikali imegawa vifaa vya Maabara na Kemikali kwa Skuli zote za Sekondari za Unguja na Pemba zenye Kidato cha Nne na cha Sita ili kuwawezesha Wanafunzi kusoma kwa vitendo na kujiandaa vyema na Mitihani yao.

Akigusia kadhia ya uvujaji wa Mitihani ya Darasa la Kumi iliyofanyika Disemba Mwaka 2018 na kupelekea Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali kufuta Mitihani hiyo Serikali tayari imeshachukuwa hatua za kuwasimamisha kazi Watendaji wote waliohusika kutoka Wizara ya Elimu pamoja na Wizara ya Habari kwa mujibu wa Sheria za Utumishi wa Umma.

Balozi Seif alisema kadhia hiyo isiyovumilika imepelekea Serikali kuiagiza Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi wa kina na kujua chanzo chake ambapo tayari imeshakamilisha kazi yake iliyoagizwa na kuwasilisha rasmi Taarifa hiyo Serikalini.

Alisema Taarifa hiyo ya uchunguzi imebaini baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar pamoja na baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kubainika kuhusiaka na kadhia hiyo iliyolitia aibu Taifa.

Balozi Seif alisema kwa mnasaba huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshalitaka Jeshi la Polisi Nchini kuwachukulia hatua za Kisheria kwa mujibu wa Makosa waliyofanya wale wote waliohusika na tukio hilo lililoleta hasara kubwa ya Fedha za Umma.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameliomba Baraza la Wawakilishi liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Hamsini na Saba, Mia Tisa na Kumi na Moja Milioni, Laki Tatu na Arubaini na Tisa Elfu { 57,911,349,000/- } kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Taasisi zake kwa ajili ya kutekeleza Program 11 kwa Mwaka wa Fedha wa 2019/2020.

Alisema katika mchanganuo huo Shilingi Bilioni Arubaini na Nane Kumi na Tatu Milioni na Laki Nne { 48,013,400,000/- } ni kwa Kazi za kawaida na Shilingi Bilioni Tisa, Mia Nane na Tisini na Saba Milioni, Laki Tisa na Arubaini na Tisa Elfu { 9,897,949,000/- } ni kwa kazi za Maendeleo.


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika kikao cha Bajeti kilichoanza rasmi Mwaka huu wa Fedha wa 2019/2020.
 Baadhi ya Manaibu Mawaziri wa Wizara za Serikali wakifuatilia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
 Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
 Baadhi ya Viongozi Waandamizi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakiongozwa na Katibu Mkuu wake Nd. Shaaban Seif Mohamed wa pili kutoka Kulia Mstari wa chini.
 Baadhi ya Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakifuatilia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyowasilishwa na Balozi Seif.
Baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakisikiliza hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyowasilishwa na Balozi Seif. Picha na – OMPR – ZNZ.