Austria imeitisha uchaguzi mpya mwezi Septemba baada ya kuvunjika kwa serikali ya muungano. Kansela Sebastiana Kurz amesema hawezi kushirikiana tena na FPÖ baada ya naibu wake kukumbwa na kashfa.

Österreich Wien PK Kanzler Kurz und Präsident Van der Bellen planen Neuwahlen (Reuters/L. Foeger)Rais wa Austria Alexander Van der Bellen amesema siku ya Jumapili kuwa anependekeza uchaguzi wa mapema wa bunge ufanyike mapema mwezi septemba kufuatia kashfa iliyoiporomosha serikali ya muungano.

“Mwanzo huu mpya unapswa kuanza haraka, haraka kadiri vifungu vya katiba ya shirikisho vinavyoruhusu, hivyo napendekeza uchaguzi … mwezi Septemba, ikiwezekana mwanzoni mwa Septemba,” alisema rais mjini Vienna, baada ya mazungumzo na kansela Sebastian Kurz.

Kurz aliitisha uchaguzi mpya baada ya mkanda wa vidio kusababisha kujiuzulu kwa kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia – Freedom Party (FPÖ) – ambacho ndiyo washirika wadogo katika muungano tawala.

Vidio hiyo iliyochukuliwa kisiri ilimuonyesha naibu kansela Heinz-Christian Strache akitoa zabuni za serikali kwa mwanamke aliedai kuwa mwekezaji kutoka Urusi, na badala yake apate upendeleo.

Kurz alisema Jumamosi kuwa hangeweza kuendelea kufanya kazi na chama cha FPÖ, akiwaambia waandishi habari kuwa amechoshwa na mlolongo wa kashfa za hivi karibuni zinazokihusisha chama hicho pamoja na ukaribu wake na makundi ya itikadi kali za mrengo wa kulia.

“Kuna hali nyingi ambamo nimeona ni vigumu kuendelea kuvumilia,” alisema Kurz.

Vidio ya kuhasirisha

Vipande kutoka mkanda wa  vidio wa masaa saba vilitolewa awali siku ya Ijumaa na jarida la habari la Ujerumani la Der Spiegel na gazeti la kila siku la Süddeutsche Zeitung.

Filamu hiyo ya siri ilimuonyesha Strache na mwenzake kutoka chamani Johann Gudenus wakizungumza na mwanamke aliedai kuwa mpwa wa tajiri wa Urusi na alikuwa anataka kuwekeza nchini Austria.

Wakati wa mkutano huo uliofanyika katika kisiwa cha Ibiza nchini Uhispania, anadaiwa kuahidi kumpa mwanamke huyo zabuni nono ikiwa atanunua gazeti la Kronez la nchini Austria, na kulitumia kusaidia chama chake katika uchaguzi wa taifa mwaka 2017.

Kwa mujibu wa machapisho hayo, Strache anamuambia mwanamke huyo kwamba hakutakuwa na upinzani wowote miongoni mwa wafanyakazi wa gazeti, kwa sababu “waandishi habari ndiyo makahaba zaidi kwenye sayari ya dunia.”

Mashirika hayo ya habari hayakueleza chanzo cha vidio hiyo, ambayo ilichukuliwa kabla ya uchaguzi wa Oktoba 2017 ambao ulishuhudia chama cha FPÖ kikiunda serikali na chama cha Kurz cha kihafidhina cha Austrian People’s Party (ÖVP).

Katika taarifa yake ya kujiuzulu, Strache alikanusha kuvunja sheria lakini alikiri kuwa alikuwa katika hali ya “kuogezeka kwa ulevi” na kwamba “alifanya kama kijana mdogo” katika jaribio la kumvutia mwenyeji wake mwenye mvuto.”

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 49 alidai kuwa alisukwa katika mpango wa mauaji ya kisiasa uliotumia kinyume na sheria mifumo ya uchunguzi.

Baada ya kuibuka kwa habari za kashfa ya vidio hiyo, kansela wa Ujerumani Angela Merkel alionya juu ya hatari ya wanasiasa ya “kuuzwa” kutoka vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia.

“Tunakabiliwa na mkondo… unaotaka kuharibu Ulaya na maadili yetu, na tunapaswa kusimama imara dhidi ya jambo hilo kwa nguvu zote,” alisema Merkel.

Tangazo la uchaguzi wa mapema limekuja siku chache tu kabla ya chama hicho cha siasa za kizalendo kilipotarajiwa kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge la Ulaya, unaoanza Mei 23.