Kingine ni mavazi mazuri ya kisichana aliyokuwa akipigilia ambayo kila msichana aliyekuwa akimtazama alikuwa akipenda kuwa kama yeye, lakini baada ya muda alipata mchumba ambaye alikuwa ni mganga maarufu jijini, Ngwizikulu Jilala na kutokomea naye nchini Botswana, ambapo alimzalisha mtoto mmoja. Nora ambaye jina lake halisi ni Nuru Nassoro, alirejea nchini baada ya kutokea kutoelewana na mzazi mwenzie huyo na kukumbwa na misukosuko mbalimbali hatimaye aliamua kurejea kwenye kuigiza tena baada ya mumewe huyo kufariki dunia kwa ajali ya gari.

Kwa sasa upepo umebadilika ameamua kuweka kila kitu pembeni na kumrudia Mwenyezi Mungu, Mikito Nusunusu limemfanyia mahojiano ya ana kwa ana kama ifuatavyo:

Mikito: Kwa nini uliamua kumrudia Mwenyezi Mungu kwa wakati huu na sio huko nyuma?

Nora: Unajua kila kitu kina wakati wake na ndivyo ilivyokuwa kwangu wakati ulikuwa bado na sasa ndio wenyewe na kuamua kufanya mengi mazuri ya kumpendeza yeye.

Mikito: Kuna mtu yeyote alikushawishi kufanya hivyo?

Nora: Hapana jambo la kumrudia Mwenyezi Mungu ni kuamua wewe mwenyewe ndani ya moyo wake mimi nilijitafakari mwenyewe na kuona hakuna starehe ambayo sijaifanya, hakuna sehemu ya starehe sijaingia hakuna nguo nzuri sijavaa sasa ni kitu gani natafuta tena?

Mikito: Zamani ulikuwa unavaa nguo zinabana na nywele zako unaziachia, vipi huoni tofauti kwa hivi sasa unavyojiziba na kubakiza macho tu.

Nora: Kama nilivyosema mwanzo hakuna ninachoona tofauti kwa sababu vitu vyote hivyo nyuma nilifanya hakuna kigeni kabisa kwangu hivyo acha muda wangu uliobaki nimtumikie Mungu.

Mikito: Kwa hiyo kwenye mambo ya uigizaji umeachana nayo?

Nora: Sidhani kama naweza kufanya zile za kidunia ila naweza kufanya ya maadili ya Kimungu na yanayotoa mafundisho kwa jamii.

Mikito: Kupitia kubadilika kwako wewe unawaambia nini wasanii wenzako?

Nora: Nawasisitizia sana kila mmoja kuwa na mwisho mzuri, kwetu hiyo ni muhimu kujiandaa na ninawashauri sana mastaa wenzangu wajitathimini vizuri kila siku na wabadilishe maisha yao kwani starehe zipo tu hazina mwisho.

Mikito: Vipi kuhusu mtoto wako, maana hujawahi kumuweka kwenye mitandao kama ilivyo kwa wengine kwa nini labda?

Nora: Hakuna sababu kufanya hivyo kwa sababu yeye sasa hivi ni mtu mkubwa hivyo ana maamuzi yake mwenyewe akitaka kufanya hivyo atafanya hivyo mwenyewe.

Mikito: Haya asante sana!

Nora: Asante na karibu.